Thursday, 20 October 2016

IRINGA KUADHIMISHWA MAADHIMISHO YA UTALII, KARIBU TANZANIA SOUTHERN CIRCUIT
MKOA wa Iringa umeanzisha mkakati wa kuhamasisha utalii wa vivutio vya kusini mwa Tanzania kwa kuwa na maadhimisho ya utalii yaliyopewa jina la Karibu Tanzania Southern Circuit.

Maadhimisho hayo yatakayohusisha mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini, yatakuwa yakifanyika mjini Iringa kila mwaka kwa kupitia mpango ambao utekelezaji wake unaanza mwaka huu.

Maandalizi ya sherehe za maadhimisho hayo yalianza jana kwa kupitia kikao kilichohusisha wadau mbalimbali kwa uratibu wa Kamati ya Utalii, Maliasili na Mazingira ya mkoa wa Iringa na Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST).

Katibu wa Kamati ya Utalii, Maliasili na Mazingira, Peter Nyakigera alisema katika kikao hicho kwamba maadhimisho hayo yatafanyika kwa mara ya kwanza mjini Iringa Novemba 27 hadi 29, mwaka huu.

Kwa kupitia maadhimisho hayo, Nyakigera alizitaja shughuli zitakazofanywa kuwa ni pamoja na kuhamasisha utalii wa ndani na kuendesha mijadala itakayoboresha shughuli za uhifadhi na utalii.

Kwa upande wake Mratibu wa SPANEST, Godwel Ole Meing’ataki alisema “tunataka kuanza kwa mafanikio makubwa, maadhimisho haya yashirikishe wadau tofauti wa ndani na hata wa nje ya nchi.”

Alisema kwa kupitia maadhimisho hayo, wanataka kuona wadau wa utalii wa mikoa hiyo wanashirikiana tofauti na ilivyosasa kwa kila mmoja kufanya mambo yake kivyake.

“Iringa na kusini kwa ujumla inakwama kiutalii kwasababu wadau wake hawana ushirikiano; hawana vyama vinavyowaunganisha wadau watu wa hoteli, watembeza watalii na wasafirishaji ili kwa pamoja waweze kushughulikia changamoto zao na za ukuaji wa sekta hiyo,” alisema.

Alisema sekta binafsi ina nafasi kubwa ya kuzifungua fursa za utalii kusini mwa Tanzania na kuchangia kukuza uchumi wa nchi na watu wake kama haitabweteka kwa kuisubiri serikali iwafanyie kila kitu.

Akifungua kikao cha maandalizi hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Wamoja Ayubu alisema mikoa ya kusini inaendelea kuzishughulikia changamoto zinazokwamisha ukuaji wa sekta ya utalii.

“Tunataka kuona kila mmoja kwa nafasi yake anashiriki kusaidia kukuza utalii. Na pale sekta ya umma inapokosea au kukwamisha mambo tuelezane ili tuyafanyie kazi,” alisema.

Alisema sekta ya utalii ina faida kubwa kwa taifa na watu wake hivyo sio sawa kuiacha iendelee kutoa mchango mdogo katika maeneo hayo kama ilivyosasa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment