Friday, 28 October 2016

DC AWAPA VYETI WALIOTAFUTA MWILI WA MWANAFUNZI ALIYEFIA MTONI
MKUU wa wilaya ya Kilolo, Asiah Abdallah amewapa vyeti vya pongezi vijana 15 walioshiriki kuutafuta na hatimaye kuupata mwili wa Frank Kastiko, mwanafunzi  wa kidato cha kwanza wa shule ya sekondari Lutangilo wilayani humo aliyefariki hivikaribuni baada ya kusombwa na maji ya mto Lukosi.

Abdallah alikutana na vijana hao ambao kati yao 10 ni wanafunzi wa shule hiyo ofisini kwake , mjini Kilolo juzi na kuwapa vyeti hivyo katika hafla fupi ya kuwapongeza iliyowashirikisha baadhi ya viongozi, walezi na walimu wa shule mbalimbali za wilaya hiyo.

“Kutokana na taarifa niliyoipata kuhusu mto na ajali ya mwanafunzi huyo, hakuna shaka kwamba kazi mliyofanya ya kuutafuta mwili wa kijana mwenzenu ilikuwa ngumu na ya kiungwana,” alisema.

Mkuu wa shule hiyo, Sebastian  Chaula alisema mwanafunzi huyo alikutwa na ajali hiyo ya maji jioni ya Julai 29, mwaka huu wakati yeye pamoja na wanafunzi wenzake watatu walipokwenda katika mto huo kufua.

Wakati wakifua, Chaula alisema taarifa za wanafunzi aliokuwa nao zinaonesha mwanafunzi mwenzao alivutwa na maji hayo na kupotea.

Alisema pamoja na kutolewa kwa taarifa za mwanafunzi huyo kupotea, watu wengi walikuwa wakiogopa kuingia katika mto huo unaodaiwa kuwa na mambo ya kimila.

“Ndipo walipojitokeza vijana hao 15 na bila woga wakaifanya kazi hiyo hadi kesho yake majira ya Saa 8.00 mchana walipoupata mwili wa mwanafunzi huyo,” alisema.

Akizungumzia mambo ya kimila yanayoelezwa kuwepo katika mto huo, Ackles Ngonyani ambaye ni mmoja wa vijana walioshiriki kuutafuta mwili huo alisema; “Taarifa za miaka mingi kijijini Kiwalamo zinasema sehemu ya mto huo kijijini hapo ni wa ajabu na una mambo ya kishirikina.”

Ngonyani alisema mto huo ambao maji yake ni ya baridi kama seruji unadaiwa kuwa na nyoka wa ajabu mwenye vichwa 12 jambo linalowaogopesha wananchi wengi wa kijiji hicho na maeneo jirani.

Ili kuepukana na maajabu hayo, walilazimika kupata maombi toka kwa wachungaji wa kijiji hicho kabla ya kuanza kuutafuta mwili wa mwanafunzi huyo.

Vijana hao walimshukuru mkuu wa wilaya kwa kutambua mchango wao katika jamii huku wakiahidi kufanya mengine mema.

Wakati huo huo, mkuu wa wilaya huyo ametoa sare kwa vijana 131 wanaoshiriki mafunzo ya mgambo ya miezi minne yanayofanyika kwa kupitia ofisi ya mgambo ya wilaya hiyo.

Abdallah alisema mgambo ni jeshi la akiba kwa ajili ya shughuli za ulinzi na usalama na akawataka baada ya kumaliza wasaidiane na wananchi katika maeneo yao kukabiliana na uhalifu.

Alisema mafunzo hayo yanatoa pia fursa ya ajira kwa vijana hao kwa kupitia utaratibu unaotoka kampunzi zote za ulinzi ziajiri watu waliopata mafunzo na kutunukiwa vyeti.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment