Wednesday, 12 October 2016

DAMU SALAMA IRINGA WAANZA NA UHABA WA VIFAA

KITUO cha damu cha hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kinakabiliwa na upungufu wa baadhi ya vifaa vilivyolezwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Robert Salim kuzorotesha kampeni ya uchangiaji damu mkoani hapa.

Kituo hicho kilichojengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 154 kwa ufadhili wa kampuni ya ASAS Ltd ya mjini Iringa, kilizinduliwa jana na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof Muhammad Bakari katika hafla iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa jengo la upasuaji.

Dk Salim alivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na mashine kwa ajili ya kutengenanisha bidhaa mbalimbali za damu, mifuko 2,000 ya kuhifadhia damu, vitanda nane vya kutolea damu, mahema manne, kompyuta nne na mashine kubwa ya kudurufu karatasi.

“Kituo hiki kilichojengwa kati ya mwaka 2014 na 2015 kilianza kazi Februari mwaka huu kikilenga kuboresha upatikanaji wa huduma za damu salama mkoani Iringa kutokana na ongezeko la mahitaji yake,” alisema.

Ili kuboresha huduma hiyo, Dk Salim alisema mkoa wa Iringa unalenga kukusanya chupa za damu 9,413 kwa mwaka ikiwa ni sawa na chupa za damu 784 kwa mwezi.

“Tangu kituo kianze kutumika mwezi Februari mwaka huu, mkoa umekusanya chupa 2,065 za damu ambayo ni sawa na asilimia 22 tu ya mahitaji yote katika kipindi hicho,” alisema.

Pamoja na uchangiaji wa damu kukwamishwa na ukosefu wa vifaa hivyo, Dk Salim alisema kituo kinakabiliwa na uhaba wa watumishi, bajeti ndogo kwa ajili ya kampeni na viburudisho kama soda, maji, biskuti, posho na usafiri kwa ajili ya kuwapa watu wanaojitolea damu.

Akizundua kituo hicho na jengo la upasuaji lililokarabatiwa kwa zaidi ya Sh Milioni 356.7 kwa ufadhili wa  hospitali ya rufaa ya Vicenza ya nchini Italia, Mganga Mkuu wa Serikali alisema miradi hiyo itachangia kufikia malengo endelevu ya kimataifa (SDGs) katika kupunguza vifo vya uzazi na watoto chini ya miaka mitano.

Kuhusu changamoto ya kutokuwa na mashine na vifaa tiba katika kituo hicho, Profesa Bakari aliushauri uongozi wa hospitali ya mkoa kuweka kipaumbele katika katika bajeti ijayo ya mpango kabambe wa hospitali.

“Napenda kuahidi kuwa wizara yangu itaweka mahitaji haya katika vipaumbele vyake na kusaidia iwapo atapatikana mhisani wa kutusaidia,” alisema huku akiwashukuru wadau waliojitolea kuboresha huduma hizo.

“Namshukuru sana ASAS kwa ujenzi wa kituo hicho na hospitali ya Vicenza kwa msaada wa ukarabati wa jengo la upasuaji na kununua samani, vifaa na vifaa tiba; tunawaomba wadau wengine wajitokeze kuchangia vifaa vinavyokosekana na miradi ya maendeleo katika hospitali hii,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment