Sunday, 11 September 2016

WANAOISHI KWA POSHO ZA WANASIASA MWISHO WAO UMEWADIASERIKALI imetangaza kuwaweka kikaangoni na ikiwezekana kuwafuta kazi maafisa ushirika wanaopokea mishahara ya kila mwezi wakati vyama vya akiba na mikopo (Saccos) katika maeneo yao vinaendelea kufa.

Akizungumza na vikundi vya wajasiriamali wanawake na vijana wa wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa juzi, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama aliwataka wakurugenzi wa halmashauri kutowafumbia macho maafisa hao ili na wao walinde vibarua vyao.

Alisema Saccos zenye matatizo ya kiutendaji zinashindwa kunufaika na mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali kwa lengo la kuwaongezea mitaji kwasababu ya kushindwa kupata msaada kutoka kwa maafisa ushirika wa maeneo husika.

“Kwa mfano hapa Mafinga najua mna Saccos ya vijana lakini kwasababu ya matatizo yake hainufaiki na mikopo hiyo na hivyo kuwaathiri wanachama wake wanaotaka kuitumia kujiletea maendeleo,” alisema.

Akihamasisha makundi mbalimbali ya jamii kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali, Mhagama amewaonya wanaotegemea posho za wanasiasa kuendesha maisha yao akisema serikali ya awamu ya tano imeanza kuufunga ukurasa huo.

“Wapo wenye nguvu za kufanya kazi lakini hawataki kujishughulisha kwasababu wanapenda na wamekuwa na utamaduni wa kuendesha maisha yao kwa kupokea vitu vya bure; baadhi yao wanashinda vijiweni asubuhi hadi jioni,” alisema.

Ikiwa imelenga kuwatoa watu hao vijiweni, Mhagama alisema serikali ya awamu ya tano inataka kuona kunakuwepo na vikundi vya wajasiriamali vyenye dhamira ya dhati ya kujiletea maendeleo kwa kuwa mipango ya kuwafikia na kuwawezesha kwa kuwapatia mikopo ipo.

Aliziagiza halmashauri kuhakikisha zinatenga maeneo yatakayotumiwa na vijana kwa ajili ya biashara au shughuli zao zingine za maendeleo.

Awali Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi alisema uanzishwaji na uendelezaji vikundi vya ujasiriamali kutasaidia kusukuma dhana nzima ya maendeleo katika wilaya nzima ya Mufindi, yenye majimbo matatu.

Hadi sasa katika halmashauri ya mji Mafinga, kuna vikundi 28 vya wajasiriamali vyenye jumla ya wanachama 5,391, mtaji wa zaidi ya Sh Bilioni 2.9, Hisa za zaidi ya Sh Milioni 420, Akiba ya zaidi ya Sh Bilioni 1.6 na amana ya zaidi ya Sh Milioni 844.


Banki ya Posta na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi waliokuwa wameandamana na waziri huyo walitoa kwa vikundi hivyo  mafunzo ya namna wanavyoweza kuzitumia taasisi hizo kuongeza mitaji yao.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment