Monday, 5 September 2016

POLISI YAKAMATA SILAHA NZITO


Jeshi la Polisi limedaiwa kukamata silaha nzito za kivita ikiwemo bunduki moja kati ya mbili zilizoporwa katika tukio la kuuawa kwa askari polisi wanne huko Mbande, katika tawi la benki ya CRDB.

Katika tukio la Mbande lililotokea hivi karibuni, polisi wanne waliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi 14 wakati wakibadilishana zamu ya lindo la benki hiyo, ambapo baada ya kuwauwa walivunja stoo na kuchukua sare za polisi pamoja na silaha.

Vyanzo mbalimbali kutoka Jeshi l Polisi vimeeleza kuwa silaha na risasi hizo zilikamatwa usiku wa kuamkia jana katika nyumba moja iliyopo Temeke, Jijini Dar es Salaam. “Baada ya tukio la Mbande polisi walianzisha operesheni kali ndipo ukasikia yale mapigano kule Vikindu.

Kuna watuhumiwa walikamatwa na katika mahojiano ndipo wakaeleza kila kitu,” kimesema chanzo hicho. Watuhumiwa hao wanadaiwa kukiri kukusanya silaha kwa kuvamia polisi ili wazitumie baadae katika matukio ya uhalifu, na kukubali kuwapeleka polisi katika ngome yao kuu.

Wakiongozwa na watuhumiwa hao, polisi walikwenda katika nyumba hiyo na wakati wakijiandaa kuivamia wakaanza kushambuliwa ambapo watuhumiwa watatu walijeruhiwa kwa risasi na baadae polisi kufanikiwa kukamata rundo la silaha zikiwemo SMG tatu, bastola 16 na Shotgun Pump Action tatu.

Katika upekuzi zaidi polisi wanadaiwa kukamata risasi 130 za Shotgun, risasi 260 za SMG, risasi 526 za bastola, radio call 12, pingu 48 na camera ya usalama (CCTV).

Hatahivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro alipoulizwa kuhusiana na taarifa hizo alisema kuwa atatoa ufafanuzi siku ya leo.


Tangu kuuawa kwa askari wanne huko Mbande, Jeshi la Polisi limekuwa likitekeleza operesheni zake za kuwatafuta wahusika na kupambana na matendo hayo kwa usiri mkubwa huku Kamishna Sirro akiahidi kutoa taarifa pale Jeshi hilo litakapohitaji kuwasiliana na Umma.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment