Thursday, 8 September 2016

MASENZA AZINDUA KAMATI YA UTALII, MALIASILI NA MAZINGIRA IRINGA


MKUU wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amezindua Kamati ya Utalii, Maliasili na Mazingira ya mkoa huo jana huku akiiagiza isaidie kuboresha shughuli za utalii katika kipindi cha miaka mitatu itakayokaa madarakani.

Ameiataka kamati hiyo inayounda na wajumbe 17 kutoka taasisi mbalimbali za uma na binafsi aliowateua yeye mwenyewe kutambua umuhimu wa ushiriki wa sekta mbalimbali katika kuendeleza utalii mkoani humo na kusini mwa Tanzania.

“Mkoa wa Iringa umeteuliwa kuwa kitovu cha utalii katika ukanda wa kusini mwa Tanzania tangu mwaka 2009. Nisaidieni jambo hili, nataka utalii ufunguke kikiwezekana zaidi ya mikoa ya kaskazini,” alisema.

Alisema matarajio ya mkoa wa Iringa katika kipindi cha miaka mitatu ya kamati hiyo ni kuona morali ya watanzania wanaotembelea vivutio mbalimbali vya utalii mkoani Iringa inaongezeka na hivyo kukuza pato la Taifa na uchumi wa wakazi wa mkoa na wawekezaji wake.

Alisema kamati hiyo imepewa jina la kamati ya utalii, maliasili na mazingita kwa kuwa wadau wanaoendeleza utalii ni wadau pia wa maliasili na mazingira, sekta ambazo ni muhimu katika shughuli hiyo.

Akiyataka majukumu mengine, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Fikira Kissimba alisema itawajibika kutoa ushauri wa kuboresha utalii na uhifadhi wa maliasili na mazingira mkoani Iringa.

Pamoja na kuwatambua wadau wanaofanya kazi katika sekta hiyo na kuwapa ushirikiano, Kissimba alisema itakuwa na wajibu pia wa kufuatilia miradi inayohusiana na utalii na uhifadhi na kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya itaibuia fursa mbalimbali za utalii na kuzitangaza.

“Kamati hii itaweka pia mikakati ya ukusanyaji wa takwimu za watalii na wawekezaji katika sekta hizo pamoja na kupokea na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoathiri maendeleo ya utalii, uhifadhi wa maliasili na mazingira,” alisema.

Pamoja na hayo yote kamati hiyo itaandaa maandiko ya kuendeleza utalii ndani ya mkoa wa Iringa na kuratibu maonesho yanayohusu sekta hiyo.


Ili kuafutilia utekelezaji wa majukumu yake kwa umakini,  Kissimba alisema kamati hiyo itakuwa ikikutana kila baada ya miezi mitatu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment