Sunday, 4 September 2016

MAHAMUDU MGIMWA ATOA MSAADA WA AMBULANCE JIMBONI KWAKE


IKIWA imepita miezi mitatu baada ya Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi kutoa msaada wa gari la kubeba wagonjwa wa jimboni kwake, Mbunge wa Mufindi Kaskazini Mahamudu Mgimwa amefuata nyayo hizo.

Mgimwa alikabidhi gari hilo lenye thamani ya Sh Milioni 80 kwa uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi katika hafla iliyofanyika katika kijiji cha Mdabulo, hivikaribuni.

Baada ya kukabidhi gari hilo, baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo walisikika wakisema wanamsubiri Mbunge wa Mufindi Kusini, Mendrad Kigola kufanya kama kilichofanywa na Chumi na Mgimwa ili kusaidia kufanikisha mikakati ya kuboresha huduma za afya katika wilaya ya Mufindi kwa ujumla wake.

Akikabidhi gari hilo, Mgimwa alisema amefanya hivyo ikiwa ni utekelezaji wa moja ya ahadi yake aliyoitoa wakati akiomba kura kwa wananchi wa jimbo hilo wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu wa 2015.

Alisema muda wa kupiga siasa umeshapita na kazi iliyopo hivi sasa ni kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuwatatulia changamoto zinazowakabili.

Alisema pamoja na kutoa gari hilo atahakikisha anashirikiana na wadau wengine wa maendeleo kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya katika jimbo lake ili kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaokwenda kutibiwa katika hospitalini ya wilaya hiyo iliyopo katika jimbo la Mafinga Mjini.

Aidha katika mkutano huo mbunge alisisitiza swala la uaminifu kwa watumishi waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi wahakikishe wanajikinga na  vitendo vinavyoashiria rushwa, vinavyoweza kuwaharibia sifa ya utendaji kazi zao na kushindwa kuwajibika ipasavyo katika majukumu yao.

Akipokea msaada wa gari hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William alisema gari hilo litasaidia kunusuru maisha ya wana Mufindi wakiwemo wajawazito na watoto hasa wale wanaohitaji kufikishwa katika hospitali ya wilaya hiyo.

Kupatika kwa gari hilo kunaifanya wilaya ya Mufindi yenye vituo 19 vya kutolea huduma kuwa na jumla ya magari matatu ya kubeba wagonjwa.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment