Tuesday, 13 September 2016

IRINGA YETU WHATSAPP YASAIDIA WATOTO YATIMA
MTANDAO wa WhatsApp unaounda kundi la Iringa Yetu la mjini Iringa umewasaidia kwa kuwapatia msaada wa vyakula na vitu mbalimbali watoto yatima wanaoishi katika kituo cha Daily Bread Life Tanzania (DBLT) cha mjini Iringa.

Mbali na mifuko minne ya unga, vingine vilivyotolewa na kundi hilo ni pamoja na unga, sukari, chumvi, sabuni, soda, juisi, miswaki, maji na nguo ambavyo kwa pamoja vimeelezwa vitawafaa watoto hao siku nyingi zijazo.

Kabla ya kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa kundi hilo, Abdukarim Mshana na baadhi ya wanachama wake waliitumia siku ya Eid el Hajj kula chakula cha pamoja na watoto hao.

“Tangu tuanzishe kundi hili miaka miwili iliyopita, tumejiwekea utaratibu wa kuzitumia siku kuu mbalimbali kutoa misaada kwa makundi mbalimbali ya watu wenye mahitaji zaidi na kula nao chakula cha pamoja,” alisema.

Alisema huo ni msaada wa pili wanautoa katika kituo cha DBLT na wataendelea kufanya hivyo katika kituo hicho na vingine huku ndoto yao ikiwa ni kutoa misaada kama hiyo kwa wafungwa wa magereza mbalimbali ya mkoani Iringa.

Katibu wa kundi hilo Janeti Kuzungula alisema kundi lao lina wanachama 48 mpaka sasa wakiwa na leengo la kuwatia faraja watoto na watu wengine wanaoishi katika mazingira hayo.

“Wito wangu kwa wanawake wenzangu wasikubali kubeba mimba kama hawajajiandaa kulea mtoto au watoto ili kuondokana na watoto wanaoingia katika mazingira magumu kwa kutupwa, kutekelezwa au kukosa mahitaji yao ya msingi,” alisema.

Alisema watoto wanaolelewa kituoni hapo na vingine vyenye sifa kama hiyo ni taifa la kesho linalohitaji kupata haki zake zote kama ilivyo kwa watoto wengine na akayaomba mashirika na watu binafsi kujitokeza kutoa misaada kama hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa kituo, mmoja wa maafisa wa kituo hicho, Tukuswiga Mwaisumbe alishukuru kundi hilo akisema msaada wao unawapa faraja watoto hao na utasaidia kupunguza gharama kubwa za uendeshaji wa kituo hicho.

Mwaisumbe alisema kituo hicho kina watoto yatima 48, ambao umri wao ni kati ya mwezi mmoja na miaka 17.

Mmoja wa watoto wanaolelewa kituoni hapo tangu mwaka 2006, William Samson alisema kwa kupitia kituo hicho amebahatika kupata huduma mbalimbali za msingi ikiwa ni pamoja na elimu.

“Nimemaliza kidato cha nne kwa msaada wa kituo hiki na sasa natarajia kujiunga na kozi ya maabara katika chuo kikuu cha Ruaha cha mjini Iringa. Na hiyo yote imewezekana kwasababu ya michango mbalimbali inayotolewa kituoni hapo na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment