Wednesday, 7 September 2016

HALMASHAURI 163 ZAFUNGA MIFUMO YA UKUSANYAJI KODI KIELEKTRONIKI

Tokeo la picha la Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Mussa Iyombe

HALMASHAURI 163 kati ya Halmashauri 185 nchini zimeunganishwa katika Mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Mussa Iyombe.

Katika hotuba yake ambayo ilisomwa na Mkurugenzi wa Idara ya uendelezaji Miundombinu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Elina Kayanda wakati wa kufunga kikao cha kumi na moja cha Mradi wa kuboresha miundombinu mijini TSCP kilichofanyika jana mjini Dodoma, Katibu Mkuu  huyo alisema serikali imejidhatiti kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato katika halmashauri zake ili kuongeza makusanyo ya mapato mara tatu ya inavyokusanya hivi sasa.

Alisema tayari Mfumo huo wa kielektroniki katika halmashauri 123 umeunganishwa na Benki ya NMB.

Mbali na Benki ya NMB, mfumo huo pia umeunganishwa na taasisi nyingine za kifedha kama vile CRDB ambapo kufikia sasa halmashauri sita zimeunganishwa, Max-Malipo, Tigo-Pesa, M-pesa, Airtel Money na taaisi nyinginezo za kifedha.

Alisema hatua hiyo itachangia ongezeko la ukusanyaji mapato ya ndani kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma na hivyo kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwahudumia wananchi wake kwa ufanisi.

Iyombe aliongeza kuwa halmashauri 140 nchini zimeunganishwa moja kwa moja na Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia mfumo wa ukusanyaji na udhibiti wa mapato kwa njia ya kielektroniki.

Kwa upande wake Mtaalamu Mshauri wa Mifumo ya teknolojia ya Mawasiliano kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bernard Mabagala alisema kuwa Wizara bado inaendelea na kazi ya kusimika mifumo ya kielektroniki katika halmashauri zilizosalia ili kuziwezesha halmashauri hizo kuboresha zoezi la ukusanyaji wa mapato.

Pamoja na kuboresha mifumo ya kielektroniki katika Mamlaka za Serikali za Mitaa Mradi wa kuboresha miundombinu mijini TSCP ambao unatekelezwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia na Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA) kufikia sasa umekwishajenga barabara za lami zenye urefu wa kilomita 141 katika miji mbalimbali nchini.

Msimamizi wa Mradi wa kuboresha miundombinu mijini TSCP kutoka Benki ya Dunia, Chyi-Yun Huang alisema kuwa Benki ya Dunia inalenga kusaidia miradi ya miundombinu nchini kwani inawagusa wananchi moja kwa moja na hivyo kuwataka watendaji wa halmashauri kufanya maandalizi ya kutosha na kuzingatia vipaumbele hivyo pindi inapoainisha miradi ya kuombea fedha.

Naye Msimamizi wa Mradi wa kuboresha miundombinu mijini TSCP wa Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA) Jemma Ngwale alielezea kufurahishwa kwake na utekelezaji wa mradi huo, ambapo amesema kuwa DANIDA inapanga kutoa zawadi kwa halmashauri tatu zilizofanya vizuri wakati wa kutekeleza mradi huo ambapo kigezo kimojawapo ni kuangalia matokeo ya utekelezaji wa shughuli za mradi huo kwa kila halmashauri.


Mradi wa Uboreshaji wa miundombinu mijini unatekelezwa katika halmashauri za miji ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Kigoma Ujiji, Tanga, na Mtwara Mikindani. Mradi huu ulizinduliwa mwezi septemba mwaka 2010 na unatarajiwa kuendelea hadi septemba 2017.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment