Monday, 1 August 2016

WATUMISHI WALA RUSHWA MAHAKAMANI KURIPOTIWA KWA SIMUMAHAKAMA ya Tanzania imezindua rasmi mpango utakaowawezesha wananchi wa mkoa wa Iringa kutumia simu zao za mkononi bila gharama yoyote kutuma taarifa za watumishi wa mahakama wa mkoani humo wanaokiuka maadili ya kazi ikiwemo kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Mkurugenzi Msaidizi wa masuala ya Utawala wa Mahakama, Wanyenda Kutta alisema mpango huo unaolenga kurejesha imani ya chombo hicho kwa jamii ni sehemu ya utekelezaji wa mambo mbalimbali yanayolenga kuboresha mfumo wa uendeshaji wa mahakama.

Aliyasema hayo juzi wakati akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza mabango yenye taarifa na namba za simu zitakazotumiwa na wananchi wenye malalamiko kutuma taarifa hizo na simu nne kwa ajili ya matumizi ya mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya za Iringa, Kilolo na Mufindi wanaounda kamati za maadili.

Alikabidhi mabango hayo siku moja baada ya watumishi wa mahakama kuu kanda ya Iringa kushiriki warsha ya siku moja iliyowapa taarifa ya kina kuhusu mpango wa maboresho ya kiutawala na kiutendaji yanayoendelea kufanywa na Mahakama ya Tanzania.

Kutta alisema mabango hayo yatabandikwa katika ofisi za serikali za ngazi zote, taasisi za umma na binafsi na sehemu zinazotoa huduma mbalimbali kwa kijamii kama hospitalini, vituo vya mabasi, taxi na bodaboda, viwanja vya michezo, mashuleni, taasisi za dini, ofisi za vyama vya siasa na sokoni.

“Katika juhudi za kupambana na rushwa mahakama imeingia katika teknolojia ya habari na mawasiliano, Tehama, ili kwa kushirikiana na wadau wake ipate mafanikio ya haraka. Wito wetu kwenu ni kutoa taarifa za kweli ili mamlaka ziweze kuchukua hatua zinazostahili kwa mtumishi aliyekiuka maadili,” alisema.

Alisema kwa kupitia namba zilizoko katika mabango hayo, taarifa za wananchi zitaifika mara moja mahakama ya Tanzania, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na kamati za maadili.

Pamoja na mpango huo, Kutta alisema maboresho hayo yamejikita katika usikilizaji wa mashauri, matumizi ya Tehama, majengo na kutumia mfumo wa Mahakama zinazotembea (Mobile court) kwa ajili ya kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi waliopo mbali na mahakama.

Akizungumzia mlundikano wa kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Ruth Masam alisema; “Mwaka jana mahakama ilikuwa na kesi za muda mrefu 48 lakini ongezeko la majaji, kutoka mmoja hadi watatu imewezesha kesi hizo kubaki tatu tu hadi sasa.”


Akipokea mabango na simu hizo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa alisema serikali ipo jirani na mahakama na akawataka wananchi kutumia fursa hiyo kutoa taarifa za kweli ili waisadie mahakama kutenda haki.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment