Friday, 19 August 2016

WATOTO WENYE VICHWA VIKUBWA NA MGONGO WAZI WAFANYIWA UPASUAJI IRINGA


WATOTO  saba kati ya 28 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi waliofikishwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa ajili ya matibabu, wamefanyiwa upasuaji.

Huduma hiyo ilitolewa kwa siku nne na madaktari wa Taasisi ya Mifupa na Upasuaji ya Muhimbili (MOI) kwa ufadhili wa taasisi ya GSM Foundation.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela waliwatembelea watoto hao juzi na kutoa wito kwa wazazi wenye watoto wenye maradhi hayo, kujitokeza ili utaratibu wa kufanyiwa matibabu uandaliwe.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa aliwataka wazazi katika wilaya yake wasihusishe magonjwa hayo na mambo ya ushirikiana akisema vyanzo vyake vinaeleweka kitaalamu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliwataka wenye watoto hao wasione aibu kujitokeza kwasababu mkoa unahitaji kujua idadi yao ili wawaombe madkatari hao warudi kwa mara nyingine kutoa huduma hiyo.

Afisa Habari wa GSM Foundation, Khalphan Kiwamba alisema taasisi yao iliamua kudhamini matibabu hayo baada ya kuelezwa changamoto yake na uongozi wa MOI.

Alisema utafiti uliofanywa na Taasisi ya MOI mwaka 2002, unaonesha zaidi ya watoto 4800 huzaliwa kila mwaka wakiwa na vichwa vikubwa na migongo wazi, na kati yao ni 500 tu wanaoweza kufika hospitali na kupata matibabu kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa madaktari.

“Taarifa zinaonesha nchi nzima ina madaktari saba tu, sita wapo MOI na mmoja yupo Bugando wakati tatizo lipo nchi nzima,” alisema.

Mmoja wa madaktari anayefanya kazi hiyo, John Mtei aliishauri serikali kuanzisha program maalumu itayowezesha madaktari wa matatizo hayo kuongezeka mafunzo kwa madaktari

Akizungumzia chimbuko la magonjwa hayo, Dk Mwanaabas Sued alisema watoto wenye vichwa vikubwa wanaweza kuzaliwa navyo au kupata siku chache baada ya kuzaliwa.

“Kwa wanaozaliwa navyo ni kwasababu ya upungufu wa virutibisho vinavyopatikana kwenye mboga za majani na matunda na kwa wanaopata baada ya kuzaliwa ni kwasababu ya maambukizi ya homa ya manjano au uti wa mgongo,” alisema.

Dk Sued alisema kwa upande wa mgongo wazi alisema husababisha watoto wapooze na kushindwa kutumia miguu yao.


“Kumchelewesha mtoto kupata matibabu ya magonjwa hayo husababisha apate mtindio wa ubongo utakasababisha ashindwe kufikia ndoto zake za maisha na kuwa mzigo kwa jamii,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment