Thursday, 4 August 2016

WAFANIKIWA KUONGEZA UZALISHAJI WA MAHINDI BAADA YA KUDHIBITI UPOTEVU

KIKUNDI cha wakulima wa kijiji cha Mangalali, Iringa Vijijini kimeongeza uzalishaji wa mahindi kutoka gunia nane hadi 20 kwa ekari baada ya kupata mafunzo ya kanuni bora za hifadhi ya mazao yaliyowawezesha kupunguza upotevu wa nafaka katika mchakato wa kuvuna hadi kuhifadhi.

Kikundi hicho chenye wanachama 184 wenye wastani wa ekari tano kwa kila mmoja, kilianzishwa mwaka 2003 kikiwa na wanachama 45.

Kilipata mafunzo hayo kupitia mradi Husishi wa kupunguza upotevu wa nafaka katika mnyororo wa thamani wa zao la mahindi unaoratibiwa na Taasisi ya Maendeleo Mijini na Vijijini (RUDI) kwa ufadhili wa taasisi ya kuleta mapinduzi yakijani barani Afrika (AGRA) inayosaidiwa na taasisi ya Rockefeller Foundation ya Marekani.

Akitoa taarifa taarifa kwa wawakilishi wa Rockefeller Foundation waliowatembelea wakulima hao hivi karibuni, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Emelita Singaile alisema kwa kupitia mradi huo wamepata pia mafunzo ya kilimo bora cha mahindi na ya matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo.

“Na tunavuna kwa kutumia maturubai yanayosaidia kupunguza uwezekano wa mavuno kupata maambukizi ya sumu kavu (aflatoxin) pamoja na punje kupotea,” alisema.

Singaile alisema mahindi wanayovuna, wanahifadhi kwa kutumia mifuko isiyoingiza hewa (PICS na AgroZ bags), Kihenge cha Chuma (metal silo) na kifukofuko (CACOON).

Meneja wa RUDI, Allan Ngakonda alisema teknolojia hizo za uhifadhi kwa pamoja inalifanya zao hilo kuwa katika hali ya usalama kwa muda mrefu zaidi bila kutumia kemikali zozote na hivyo kusaidia kulinda afya za walaji.

Baika Kindole ambaye ni mkulima mwanachama wa kikundi hicho alisema; “ zamani tulikuwa tunavuna kwa kulundika mahindi chini na kuyapukuchukua katika mazingira yaliyokuwa yanaongeza upotevu.”

“Tunaishukuru Rockefeller Foundation na AGRA kwa kuiwezesha RUDI kifedha na RUDI kutuwezesha kupata teknolojia mpya na kutuunganisha na mnunuzi wa uhakika wa zao la mahindi ambaye ni Basic Element,” alisema.

Meneja wa RUDI alisema kabla ya mradi kuja na matumizi ya teknolojia hizo, wakulima walikuwa wanapoteza asilimia kati ya 25 na 40 ya mazao wanayovuna.

“Upotevu umepungua hadi asilimia 15 na baada ya miaka miwili kutoka sasa tuna hakika hakutakuwa na upotevu wowote wa nafaka kwasababu matumizi ya teknolojia hizo yanazidi kuongezeka,” alisema.

Aliwataka wakulima wote nchini kuingia kwenye matumizi ya tekenolojia mpya ya kuhifadhi mazao, ili wapate tija katika kile wanachozalisha.

“Na katika kuongeza uzalishaji, wakulima tunawahamasisha kutumia mashine za kupukuchua mahindi zinazopatikana kwa bei ndogo badala ya kutumia njia za kale za kupiga mahindi kwa fimbo,” alisema.

Alisema  kwa kupitia mradi huo RUDI inafanya kazi kazi na vikundi 42 vinavyojihusisha na kilimo cha mahindi katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tangu tuanze kutekeleza mradi huo wa AGRA na mingine                         tumekwishawafikia wakulima zaidi ya 75,000,” alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment