Saturday, 6 August 2016

SPUTANZA MKOA WA IRINGA YAVUKA VIUNZI NA KUPATA VIONGOZI WAKE WAPYA


MKOA wa Iringa umefungua ukurasa mpya wa mikakati yake ya kuinua soka la mkoa huo baada ya wanachama wa Chama cha Wanasoka Tanzania (SPUTANZA) mkoani humo kupata safu yake mpya ya uongozi inayounda kamati ya utendaji ya chama hicho mkoa wa Iringa.

Uchaguzi huo ulioratibiwa na mwanachama wa kudumu wa SPUTANZA Taifa, mwanamichezo na mfanyabishara maarufu wa mjini Iringa, Feisal Asas umefanyika jana ikiwa ni zaidi ya miaka nane tangu uchaguzi wa mwisho wa chama hicho ufanyike mkoani hapa.

Katibu Mkuu wa SPUTANZA Taifa Said George na maafisa utamaduni na michezo wa halmashauri za wilaya za Kilolo na Manispaa ya Iringa walijitokeza kushuhudia uchaguzi huo wa kihistoria uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Isimila mjini Iringa.

Jumla ya wanachama 57 walipiga kura kuwachagua viongozi hao katika uchaguzi huo uliosimamiwa na kamati ya uchaguzi ya wajumbe watano waliongozwa na mwenyekiti wake, Wakili Barnabas Nyalusi.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo ambao wagombea wake wote hawakuwa na upinzani, Nyalusi alisema wakati nafasi ya Mwenyekiti ilikwenda kwa David Masasi, mkutano huo ulimchagua Abou Silia kuwa Makamu Mwenyekiti.

Mchazaji wa zamani wa Lipuli FC ya mjini Iringa, Haji Mambo alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu huku Julio Mgonja akichaguliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu.

Nyalusi alimtangaza Nazalius Msilu kuwa Mweka Hazina wa SPUTANZA mkoa wa Iringa huku mshambuliaji wa zamani aliyepata kuwika na timu mbalimbali za soka nchini, Lisa Mwalupindi akichaguliwa kuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa SPUTANZA Taifa.

Dickson Kiboye, Hamid Mbatta na Haji Mwilima walichaguliwa kuwa wajumbe wa kamati tendaji ya SPUTANZA mkoa huku nafasi mbili zikiachwa wazi baada ya walioomba kukosa sifa.

Awali mwanachama wa kudumu wa SPUTANZA, Feisal Asas aliuahidi uongozi mpya kuwapa msaada wutakaowawezesha kuanzisha ligi ya SPUTANZA itakayoshirikisha mikoa ya nyanda za juu kusini.

“Kwa kushirikiana na vyma vya mpira, hatua hiyo itausaidia mkoa wa Iringa kupiga hatua nyingine ya maendeleo ya soka,” alisema.

Katibu Mkuu wa SPUTANZA Taifa ameahidi kuupa ushirikiano wa kutosha uongozi mpya wa SPUTANZA mkoa wa Iringa ili ufikie malengo yake.

Mwenyekiti mteule ambaye msomi mwenye shahada mbili za chuo kikuu aliahidi kushirikiana na wadau wengine wa soka wa mkoa wa Iringa kushughulikia changamoto za mchezo huo ili kurudisha hadhi yake.

Mwenyekiti mstaafu wa SPUTANZA, July Sawani alikirushia lawama Chama cha Mpira wa Miguu wa Mkoa wa Iringa (IRFA) akisema kinachangia kuzorotesha maendeleo ya soka ya mkoa huu kwasababu ya ubinafsi wa baadhi ya viongozi wake.

“Kwa miaka mingi IRFA imekuwa ikiongozwa na viongozi wanaojali maslai yao na wanaofanya kila wawezalo ili wabaki madarakani. Viongozi hao hawana mpango na vyama vingine vya mpira huo kwa hofu tu ya kupoteza nafasi zao,” alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment