Tuesday, 16 August 2016

SPANEST YAWASAIDIA ASKARI WANYAMAPORI WA MBOMIPA
MRADI wa Kuimarisha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST) umetoa msaada wa vifaa vyenye thamani ya Sh Milioni 16.3 kwa askari wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Tarafa ya Idodi na Pawaga (Mbomipa) inayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ili kuboresha doria dhidi ya majangili.

Katika eneo hilo la ukubwa wa kilomita za mraba 776.4 kuna wanyamapori wa aina mbalimbali wanaoingia na kutoka  katika hifadhi hiyo na hifadhi ya Taifa ya Mikumi hali inayowaweka katika hatari ya kushambuliwa na majangili.

Vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 16 vilikabidhiwa juzi mjini Iringa katika kikao ambacho jumuiya hiyo ilikitumia kukutana na wadau wake mbalimbali kujadili na kuzipatia utatuzi wa muda mfupi na mrefu wa changamoto zake mbalimbali zinazoikabili.

Mratibu wa SPANEST, Godwel Ole Meing’ataki alivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na buti za kisasa 48, sare za ulinzi 48, mikanda 48, soksi 48, kofia 48, Tochi 10, filimbi 10, Kamba 24, masweta 24 na makoti ya mvua 24.

Meing’ataki alisema vifaa hivyo vitasaidia kuimarisha kikosi cha doria cha jumuiya hiyo ili kukidhi haja ya kitaifa na kimataifa ya kulinda wanyamapori na rasilimali zingine za Taifa katika eneo hilo la Mbomipa kama inavyotakiwa kufanywa katika maeneo yote yaliyohifadhiwa nchini.

Mwenyekiti wa Mbomipa, Christopher Mademla alisema kabla ya kupatiwa vifaa hivyo, askari wa jumuiya hiyo walikuwa wakifanya doria kwa kutumia vifaa hafifu visivyo na hadhi ya kijeshi jambo lililosababisha wakati mwingine washindwe kutofautishwa na majangili

“Askari wetu walikuwa wanavaa mavazi ya kawaida na makobasi ambayo ni aina ya ndala zinazotengenezwa kwa tairi chakavu za magari. Mavazi hayo yaliwafanya wakati mwingine wadhaniwe ni majangili na kujikuta wakikamatwa na askari wa TANAPA,” alisema.

Alisema Mbomipa ina askari 27 waliopata mafunzo huku wengine 24 wakiandaliwa kwa ajili ya kupelekwa mafunzoni mkoani Ruvuma na kwamba kupatikana kwa vifaa hivyo kumesaidia kubadili sura ya jumuiya hiyo dhidi ya vita ya ujangili.

Kuhusu silaha alisema, wamekwishapata kibali cha kutumia silaha za moto katika doria zao hatua itakayofutilia mbali silaha duni (virungu na mapanga) walizokuwa wakizitumia kukabiliana na majangili.

Akiwakabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema uwepo wa Mbomipa katika eneo hilo ni muhimu katika kulinda rasilimali zilizopo ndani yake pamoja na kupunguza umasikini wa vijiji vinavyounda jumuiya hiyo.

“Mna wajibu wa kuunga mkono juhudi za serikali za kuokoa wanyamapori hasa Tembo anayewindwa mchana na usiku na majangili. Tumieni vifaa mlivyopewa hii leo kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment