Thursday, 18 August 2016

PROGRAMU YA KUPIGA MSWAKI MASHULENI YAZINDULIWA WILAYANI IRINGA


WANAFUNZI wa baadhi ya shule za msingi za halmashauri ya wilaya ya Iringa wameanza kutekeleza program ya upigaji mswaki mashuleni inayolenga kuwafanya wawe na afya njema ya kinywa na mwili.

Uzinduzi wa programu hiyo inayojulikana kwa jina la FIT FOR SCHOOL ulifanywa jana na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Halfani Lulimi katika shule ya msingi Mgama.

Pamoja na upigaji mswaki kwa kutumia dawa yenye madini ya floraidi, program hiyo inajumuisha pia unawaji mikono kwa makundi kwa maji tiririka na sabuni na umezaji wa dawa za minyoo ambazo hutolewa mara mbili kwa mwaka.

Afisa Afya wa Halmashauri hiyo, Samwel Oberlin alisema program hiyo inayojumuisha mambo hayo matatu inafadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa kuanzia inatekelezwa katika shule za msingi nane za Mgama, Magunga, Makongati, Mtera, Makatapola, Kinyali na Kihanga.

“Dhumuni kubwa la program hii ni kufanya mazingira ya shule yawe bora kiafya na kitaaluma na kuwafanya wanafunzi kupenda kufanya matendo ya kiafya kwa pamoja wakiwa shuleni ili wajijengee mazoea ya kufanya vitendo hivyo wakiwa pekee yao ndani na nje ya shule,” alisema.

Akizindua program hiyo, Lulimi alisema ili program hiyo itekelezwe kwa uhakika ni lazima mifumo ya maji katika shule hizo itunzwe na akazitaka shule ambazo haziko katika mradi ziangalie namna zinavyoweza kutekeleza program hizo kwa kutumia gharama nafuu.

Awali Mratibu wa Afya Mashuleni wa halmashauri hiyo (SWASH), Kokubelwa Samlelwa alisema toka mwaka 2013 halmashauri hiyo imeendelea kutekeleza kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira inayohusisha ngazi ya kaya na shule.

“Moja ya kishiria muhimu katika ngazi ya shule ni uwepo wa kifaa cha kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni,” alisema.

Alisema kwa kushirikiana na UNICEF kampeni hiyo inafanywa katika kata tano za Maboga, Kihanga, Mgama, Izazi na Migoli.

Alizitaja shughuli zilizofanywa kupitia kampeni hiyo kuwa ni pamoja na uhamasishaji, mafunzo, ujenzi wa majengo 26 ya vyoo katika shule za msingi 14, upatikanaji wa maji safi katika shule 13 na ujenzi wa miundombinu ya kunawa mikono katika shule 11.

Samlelwa aliyataja mafanikio yaliyotokana na shughuli hizo katika kipindi cha Julai 2012 na Juni 2016 ni pamoja na asilimia ya wanafunzi wanaopata huduma ya vyoo bora kuongezeka kutoka asilimia 11 hadi asilimi 8 na, wanaopata huduma ya maji safi katika mazingira ya shule wameongezeka kutoka asilimia 30 hadi asilimia 80.

Kwa upande wa kaya zenye vyoo bora zimeongezeka kutoka asiliami 14 hadi asilimia 44 huku kaya zenye kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni ikiongezeka kutoka asilimia 25 hadi 46.


Mkuu wa shule ya Msingi Mgama, Boaz Ngalutila aliishukuru halmashauri hiyo na wadau wake wa maendeleo kwa kuanzisha program hiyo shuleni hapo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment