Saturday, 6 August 2016

MWENYEKITI WA CCM MKOA WA IRINGA KUTOA BURE MAFUNZO YA UJASIRIAMALI


MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Dk Jesca Msambatavangu amesema yupo tayari kuwawezesha vijana kuwa na ujuzi wa kutengeneza mipango ya biashara zao ili wadumu kwa muda mrefu katika sekta hiyo kwa mafanikio.

“Ofa hii naitoa kwa vijana na makundi mengine mbalimbali ya kijamii mkoani Iringa kwa ajili ya kubadili mwenendo wa biashara na maisha yao,” alisema.

Akizungumza na wanahabari hivikaribuni, Dk Msambatavangu alisema wajasiriamali wengi wana tatizo kubwa la mafunzo jambo linalowafanya wakose ubunifu na hivyo kuhatarisha shughuli zao.

Alisema pamoja na biashara kuonekana kuwa kimbilio la wengi, sio wote wanaoingia  huko na kuwa wajasiriamali wanafanikiwa.

“Tafiti zinaonesha baadhi ya biashara zinazoanzishwa zinakufa mwaka mmoja baada ya kuanzishwa na baadhi ya zile zinazovuka kipindi hicho, hufa baada ya miaka mitano,” alisema

Alisema biashara nyingi zinakufa kwasababu wahusika wake hawana elimu muhimu ya biashara, ujasiriamali na mipango yake kwani wamekuwa wakiingia katika shughuli hiyo kwa kuangalia watu wengine wanachofanya.

“Wewe kama mjasiriamali au unataka kuingia kwenye ujasiriamali una jukumu la kujifunza mipango ya biashara na kufuata misingi yake ili uweze kufikia malengo yako,” alisema.

Alisema anataka wajasiriamali wawe na mipango ya biashara zao itakayowawezesha kujipanga kutoka sasa ili baada ya muda fulani malengo wanayojiwekea yaweze kuonekana.

“Ukiwa na mipango itakuwa rahisi kujua baada ya muda fulani utakuwa wapi, vinginevyo utakuwa ukifanya ujasirimali kwa miaka yote bila kukupa mafanikio yoyote,” alisema.

Mbali na vijana, aliyaalika makundi mengine ya kijamii mkoani hapa kama bodaboda, vikundi vya akina mama, wazee, wanahabari na watumishi wanaotaka kuwa wajasiriamali kupata mafunzo hayo.

Msambatavangu ambaye ni msomi katika fani ya biashara aliyewekeza katika sekta ya elimu na huduma za fedha alisema mafunzo hayo anayatoa bila gharama yoyote kwa makundi yatakayokuwa tayari.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment