Sunday, 14 August 2016

MKUU WA MKOA IRINGA ATEMBELEA KAYA MASIKINI IRINGA VIJIJINI

ZAIDI ya Sh Bilioni 2.3 zimeingia katika mzunguko wa fedha wa Iringa Vijijini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaorataibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Sehemu ya fedha hizo zimetumiwa na kaya hizo kuanzisha miradi midogo ya ufugaji, kilimo, ujenzi na vikundi vya kuweka na kukopa, maarufu kama Vicoba.

Mratibu wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Iringa Vijijini, Christopher Kajange alisema jumla ya kaya 8,439 kutoka katika vijiji 82 kati ya vijiji 133 vya wilaya hiyo zinanufaika na mpango huo ulioanza kutekelezwa Julai, mwaka jana.

Kajange alisema fedha hizo zimeziwezesha zaidi ya kaya 4,000 kati ya kaya hizo zilizopo katika mpango kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na hivyo kujihakikishia kupata huduma za matibabu kwa mwaka mzima bila malipo yoyote.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza juzi alizitembelea baadhi ya kaya zinazonufaika na mpango huo katika kata ya Izazi na Migori na kueleza jinsi alivyoridhishwa na utekelezaji wa mpango huo unaolenga kuzikomboa kaya masikini.

“Mradi unalenga kusaidia kaya hizi ili ziondokane na umasikini, mkiongeza kasi ya kujiwekea akiba kwa kila gawio mnalopata, baada ya muda fulani wote mtajikuta katika mazingira ya kuboresha shughuli zenu nyingine za maendeleo,” alisema alipokuwa katika kijiji cha Izazi.

Masenza alitaja eneo lingine linaloweza kuzisaidia kaya hizo kujiongezea kipato kuwa ni la kilimo cha mbogamboga ambazo mahitaji yake yanaongezeka siku hadi siku kwa sababu ya umuhimu wake kiafya.

Akiwa katika kijiji cha Makatopola kata ya Migori, Mkuu wa Mkoa alitembelea nyumba ya Damalis Mdabaga ambaye ni mmoja wa wanawake wanaonufaika na mpango huo na kuiagiza halmashauri ya wilaya ya Iringa imsaidie bati 15.

Aliitaka halmashauri hiyo kutoa bati hizo baada ya mtoto wa mama huyo, Kweginansi Kafulu kuahidi kuijenga upya nyumba hiyo ndogo ya udongo iliyobomokabomoka kila mahali kwasababu ya uchakavu wake.


Akiahidi kutekeleza agizo la mkuu wa mkoa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robert Masunya alisema mpango huo ni muhimu kwa vile unawezesha kaya za walengwa kupata kipato zaidi, unatengeneza fursa zingine  na unawapatia walengwa weledi na stadi za mbalimbali wakati wa utekelezaji miradi.

“Utekelezaji wa mpango huu haulengi tu katika kuhawilisha fedha kwa walengwa bali pia unahimiza ushiriki wa walengwa katika kazi za mikono kupitia miradi ya mbalimbali katika maeneo yao ili waweze kupata kipato, na kuwekeza" alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment