Monday, 1 August 2016

MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA NAYO YAMTEMBELEA ALIYETENGENEZA CHOPA


Hatimaye Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imemtembelea Mkazi wa Tunduma Mkoani Songwe, Adam Kinyekile aliyetengeneza helikopta ikiwa ni siku chache baada ya mtaalam huyo kutembelewa na Raia wa Kigeni (Wazungu) kutoka nchini Afrika Kusini na kupatiwa mualiko maalum wa kutembelea kiwanda chao cha helikopta nchini humo.

Kinyekile ambaye pia ni fundi magari amesema ujumbe wa maafisa wanne kutoka TCAA Makao Makuu ulifika ofisini kwake kwa ajili ya kuikagua helikopta hiyo.

Amewataja maafisa hao kuwa ni pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Uendeshaji wa Ndege, Kapteni Kintu Newa, Mkaguzi Mkuu wa Usalama wa Ndege, Majaliwa Burhan, Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ubora wa Ndege, Abdillah Mfinanga na Meneja wa TCAA­Mbeya, Victor Calson. Mmoja wa maafisa hao, Burhan alikiri kumtembelea fundi huyo lakini alikataa kutoa maelezo zaidi huku Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari akisema kuwa hawawezi kuzungumzia jambo hilo kwa undani sana hadi pale maafisa waliotumwa watakaporejea wakipitia kwanza Mkoani Arusha kikazi na baadae kurejea Dar es Salaam.

Awali Mamlaka hiyo ilitoa onyo kali kwa yeyote Yule anayejihusisha na uundwaji wa ndege bila kufuata utaratibu au kuwaona wao, onyo ambalo lilihisiwa na wengi kuwa lilimlenga Kinyekile ambaye ndiye alikuwa ametoka kutengeneza chopa hiyo iliyowekewa jiwe la msingi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge alipokuwa Tunduma.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment