Friday, 5 August 2016

LISSU ALALA RUMANDE, KUPANDISHWA KIZIMBANI TENA LEO


Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Tundu Lissu amejikuta akitumia usiku wa kuamkia leo rumande baada ya Jeshi la Polisi, kanda Maalumu ya Dar es Salaam kumnyima dhamana baada ya kumaliza kumhoji katika kituo kikuu cha polisi licha ya viongozi wa chama hicho kufurika kituoni hapo kwa ajili ya kumdhamini.

Baadhi ya viongozi waliofika kumwekea dhamana ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mjumbe wa Kamati Kuu, Edward Lowassa, aliyefika saa 12:14 jioni akiungana na viongozi na wanachama wengine wa chama hicho.

 Baada ya kufika Lowassa, wanachama na wafuasi wa Chadema waliokuwa nje ya ofisi hizo za polisi walianza kuimba wimbo wa kumuita rais, rais, rais ikiwemo na kauli mbiu ya maarufu ya People’s Power na kupokelewa na Mbowe na Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob waliokuwa nje ya geti.

Viongozi hao waliokuwa nje baada ya kuzuiwa kuingia ndani na polisi waliongozana na Lowassa kuomba kuingia lakini walizuiwa hali iliyofanya wachukue uamuzi wa kuondoka na mtu pekee aliyeruhusiwa kuingia alikuwa ni Meya wa Dar es Salaam, Isaya Mwita.

Naye Mwanasheria wa Lissu, Peter Kibatala alisema kwamba mahojiano kati ya jeshi hilo na mtuhumiwa yalianza saa 9:30 hadi saa 12:30. “Katika maelezo ya polisi wanasema kwamba wakati Lissu akitoka mahakamani juzi kwenye kesi yake alitamka maneno ya uchochezi, lakini haya yote yanahitaji ushahidi,” alisema Kibatala.


Wakili huyo alisema kwamba polisi baada ya kumaliza mahojiano na wao wakiwa wameandaa utaratibu wa dhamana walikataliwa hadi leo Ijumaa atakapofikishwa mahakamani.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment