Thursday, 4 August 2016

KAYA MASIKINI KILOLO ZAGEUKIA KILIMO CHA MITI YA MBAO
BAADHI ya kaya masikini za wilayani Kilolo mkoani Iringa zimeanza kuwekeza katika kilimo cha miti ya mbao kwa kutumia akiba ya fedha wanazopata kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaorataibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Pamoja na kilimo hicho, kaya hizo zimeanzisha ufugaji mdogo wa kuku, mbuzi na nguruwe hatua waliyosema inalenga kuwaongeza uhakika wa chakula na mapato ili waondokane na umasikini.

Mratibu wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Kilolo, Venance Mwaikambo alisema jumla ya kaya 6,401 kutoka katika vijiji 70 vya wilaya hiyo wananufaika na mpango huo ulioanza kutekelezwa Julai, mwaka jana.

“Tayari mpango umemaliza mwaka mmoja, na mwezi huu tumeingia rasmi mwaka wa pili wa utekelezaji wa mpango huu kwa kuendelea kutoa fedha kwa kaya hizo kwa kupitia zoezi lililoanza juzi,” alisema.

Afisa ushauri na ufuatiliaji wa mpango huo wa TASAF wilayani Kilolo, Happy Mpuya alisema mpango huo ni muhimu kwa vile unawezesha kaya za walengwa kupata kipato zaidi, unatengeneza fursa zingine za ajira,  na unawapatia walengwa weledi na stadi za mbalimbali wakati wa utekelezaji miradi.

“Utekelezaji wa mpango huu haulengi tu katika kuhawilisha fedha kwa walengwa bali pia unahimiza ushiriki wa walengwa katika kazi za mikono kupitia miradi ya mbalimbali katika maeneo yao ili waweze kupata kipato, na kuwekeza" Mpuya alifafanua.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wa utekelezaji wa mpango huo, zaidi ya Sh Bilioni 1.3 zimetumika kuziwezesha kaya hizo ambazo kila baada ya miezi miwili zimekuwa zikijipatia kati ya Sh 20,000 na Sh 70,000 kulingana na vigezo mbalimbali vya umasikini.

Mmoja wa wanufaika wa mpango huo, Alphonce Kimung’e wa kijiji cha Idete alisema baada ya kufiwa na mkewe aliyemuachia watoto saba alikuwa katika hali ngumu ya kimaisha yaliyoanza kubadilika baadaye baada ya kuingizwa katika mpango huo unaomuwezesha kupata Sh 50,000 kila baada ya miezi miwili.

“Kwa akiba niliyokuwa najiwekea kutoka katika kiasi hicho cha fedha, nimeanzisha ufugaji wa kuku lakini pia nina ekari moja na nusu ya miti ya mbao,” alisema.

Naye Anyamisye Kikoti wa kijiji cha Itonya alisema kwa kutumia fedha hizo amekodi ekari mbili ya shamba na kupanda miti.

“Ekari moja ya shamba inachukua wastani wa miti 600. Na wastani wa bei ya mti mmoja uliokomaa kwasasa ni Sh 20,000. Kwahiyo baada ya miaka nane endapo shamba langu halitapata tatizo lolote, kwa bei ya sasa nitakuwa na uhakika wa kupata Sh Milioni 24,” alisema.

Kwa upande wake,Huruma Mville wa kijiji cha Uluti alisema hali ya maisha ya familia yake yenye watoto saba imebadilika baada ya kuingia katika mpango huo.

“Katika kujiongeza nilinunua nguruwe mmoja ambaye sasa ana mimba, atakapozaa, fedha nitakazopata nitatumia kukarabati nyumba yetu ambayo kwa kweli ipo katika hali mbaya,” alisema Mville ambaye pia mumewe ni mlemavu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment