Monday, 1 August 2016

CHADEMA YASISISTIZA KUIFANYA OPARESHENI YAKE MPYA YA UKUTA


Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema licha ya viongozi wa chama hicho kutishwa, kukamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi, bado msimamo wao kuhusu operesheni Ukuta itakayofanyika Septemba Mosi mwaka huu uko pale pale

Lissu ameyasema hayo jana Jijini Dar es Salaam baada ya kuhojiwa na kuachiwa kwa dhamana kwa Mwenyekiti wa Taifa Chadema, Freeman Mbowe na kudai kuwa msimamo wao uko palepale na hakuna kilichobadilika.

 “Wamemuhoji kwa taarifa aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari juu ya msimamo wa chama wa kufanya mkutano nchi nzima. Tatizo jeshi letu wakisikia maandamano, mkutano au mtu anamsema Magufuli basi anatuhumiwa kwa uchochezi, wametumia muda mrefu kumuhoji lakini mwisho wamemwachia kwa dhamana na watamuita pale watakapomhitaji tena,” amesema Lissu.

Ameongeza kuwa ni muhimu sana huko tunapoenda kuzungumza na wenzetu hii kitu inaitwa uchochezi ni nini? Tunashitakiwa kwa sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo waliingiza vifungu vya uchochezi mwaka 1978 lengo lao kuu ni kuwafunga watu midomo na ilitungwa wakati wa mfumo wa chama kimoja.

 Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), amesema kuitwa mchochezi, ni jambo la ufahari kupinga udikteta kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere.

Amesema pamoja na hayo bado msimamo wa chama hicho kufanya mikutano waliyoiita Operesheni Ukuta ipo pale pale ifikapo Septemba Mosi, mwaka huu. Chama hicho kinatarajiwa kufanya operesheni mpya iliyopewa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) itakayokwenda sambamba na uzinduzi wa mikutano ya hadhara nchi nzima, ambayo itafanyika Septemba Mosi, mwaka huu.

Mbowe alifika kituoni hapo akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali wa Chadema akiwamo Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa ambaye hata hivyo alizuiwa kuingia katika chumba cha mahojiano.

Askari waliokuwa kwa wingi katika eneo hilo, walisikika wakisema kuwa anayepaswa kuingia ndani ni Mbowe, Mwanasheria Tundu Lissu na Wakili wa Chadema, John Mallya.

Lowassa, wafuasi wa Chadema na waandishi wa habari walilazimika kubaki nje huku askari wakiimarisha ulinzi wakiwa wamebeba bunduki zao huku magari yenye maji ya kuwasha yakiwa yameegeshwa pembeni.


 Wakati chama hicho kikijiandaa kutekeleza Operesheni Ukuta Septemba Mosi, tayari Rais Magufuli amezuia operesheni hiyo na kuwaonya wale wote watakaokaidi agizo lake na kuamua kuandamana.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment