Sunday, 31 July 2016

WORLD SHARE YA KOREA YAINGIA USHIRIKIANO NA OFISI YA MBUNGE WA MAFINGA MJINI

OFISI ya Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini imeingia makubaliano ya ushirikiano na taasisi ya World Share ya Korea ambayo hapa nchini inatoa misaada mbalimbali ikiwemo ya uchimbaji wa visima, ujenzi wa matenki na mifumo yote ya maji, kusadia watoto yatima na watu wenye ualbino na kutoa msaada wa taa zinazotumia sola.

Makubaliano yamefanyika jana ikiwa ni siku moja tu baada taasisi hiyo kuahidi kushughulikia tatizo la maji katika shule ya msingi ya Makalala Mchanganyiko ya mjini Mafinga.

Akitoa ahadi hiyo mbele ya Balozi wa Korea nchini, Song Geum Young aliyetembelea jimbo hilo kwa mwaliko wa mbunge wake, Cosato Chumi, afisa wa taasisi hiyo Nara Kim alisema:

“Tutatoa msaada huo kama tutahakikishiwa kuondolewa vikwazo vya askari wa usalama barabarani wakati tukisafirisha mtambo wa kuchimba visima toka Dar es Salaam.
 
Alisema taasisi hiyo inayofanya kazi zake nyingi jijini Dar es Salaam inahofia kupata kadhia kutoka kwa askari hao kama inavyotokea mara kwa mara katika jiji hilo.

Akizungumzia tatizo la maji shuleni hapo, mkuu wa shule hiyo Shem Muheni alisema linaongeza mateso kwa wanafunzi hao wakiwemo wenye ulemavu wanaokabiliwa na changamoto nyingine ya uchakavu wa miundombinu ya mabweni na mazingira rafiki ya kusomea.

Muheni alisema hiyo ina wanafunzi 548 na kati yake 85 wana ulemavu tofauti ukiwemo wa viungo, akili, ngozi, macho na vichwa vikubwa.

Akishukuru kwa ahadi ya taasisi hiyo, Mbunge Chumi aliahidi kuzungumza na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Mohamed Mpinga ili kuona namna taasisi hiyo kwa kuzingatia sheria za barabarani itakavyosaidiwa ili itekeleze ahadi  hiyo.

“Nimshukuru Chumi kwasababu bila ombi lake huenda nisingefika Mafinga hii leo na kusingekuwa na makubaliano na misaada hii,” alisema Balozi wa Korea wakati akizungumza na jumuiya ya shule hiyo na kaya za kijiji cha Mtula.

Mbali na kukabidhi msaada wa mafuta maalumu ya ngozi kwa wanafunzi wenye ualbino katika shule hiyo, alikabidhi msaada wa taa 400 zinazotumia mionzi ya jua zilizotolewa shuleni, zahanati ya Mtula na kwa kaya masikini katika kijiji cha Mtula, Bumilainga na Itimboa.

Katika ziara hiyo, balozi huyo pia alitembela skimu ya umwagiliaji ya Mtula inayoendesha na chama cha Ushirika cha Mtula chenye wanachama 68 huku ikinufaisha kaya 390 za kijiji hicho cha Mtula.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment