Saturday, 16 July 2016

Shule ya kata yafanya kweli


BARAZA la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya Kidato cha Sita 2016, ambayo ufaulu wake umeshuka, huku shule ya sekondari Kisimiri, ambayo ni ya kata ikishika nafasi ya kwanza kitaifa.
Shule hiyo iliyoko Arumeru mkoani Arusha, imeongoza shule zilizozoeleka katika nafasi za juu na zinazofahamika kwa kutoza ada bei ghali, pamoja na shule kongwe za serikali, ambazo hata hivyo zimeonesha kurejesha makali yake.
Akitangaza matokeo hayo jana, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, alisema ufaulu wa jumla katika mtihani wa kidato cha sita mwaka huu, umeshuka kwa asilimia 0.93 ikilinganishwa na mwaka 2015, ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 98.87. Mwaka huu ni asilimia 97.94.
“Hata hivyo, ubora wa ufaulu unazidi kuimarika kwa kuwa na idadi ya watahiniwa waliofaulu vizuri katika daraja la kwanza, pili na tatu, umeongezeka kwa asilimia 3.72 kutoka asilimia 89.41 mwaka 2015 mpaka asilimia 93.13 mwaka 2016,” alisema.
Alisema jumla ya watahiniwa 71,551, sawa na asilimia 97.32 ya watahiniwa 73,940 waliofanya mtihani huo wamefaulu; kati ya hao wasichana ni 26,977 na wavulana ni 44,574. Dk Msonde alisema watahiniwa wa shule waliofaulu ni 63,528 ambao ni asilimia 97.94 ya watahiniwa wote waliofanya mtihani, wasichana wakiwa ni 24,062 na wavulana ni 39,466.
*Ubora wa ufaulu
Akizungumzia ubora wa ufaulu, Msonde alisema watahiniwa 60,407 sawa na asilimia 93.13 wamefaulu katika daraja la I hadi III wakiwemo wasichana 23,045 na wavulana 37,362.
“Watahiniwa 6,272 wamepata daraja la kwanza, 27,125 daraja la pili, watahiniwa 27,010 daraja la tatu. Watahiniwa 60,407 wamepata daraja la IV huku watahiniwa 1,333 wakifeli kwa kupata daraja sifuri,” alisema.
*Shule bora
Dk Msonde alitaja shule iliyoongoza kwa kushika nafasi ya kwanza kuwa ni shule hiyo ya sekondari Kisimiri ya Arusha.
Taarifa zinaonesha kuwa, shule hiyo ya kata hii ni mara ya tisa kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha sita na katika awamu zote hizo, iliingia katika kumi bora mara tano na kati ya hizo, iliingia katika tatu bora mara mbili na matokeo ya mwaka huu, imeingia katika tatu bora mara ya tatu; ikiongoza shule zote nchi nzima.
Shule ya pili ni Feza Boys ya Dar es Salaam, ikifuatiwa na Alliance Girls (Mwanza), Feza Girls (Dar es Salaam) huku shule kongwe ya serikali ya Tabora Boys (Tabora), ikishika nafasi ya tano kitaifa.
Nyingine ni Marian Boys ikifuatiwa na shule nyingine kongwe ya serikali ya Kibaha, zote za mkoani Pwani, kisha Mzumbe (Morogoro) ambayo pia ni kongwe ya serikali, Ilboru (Arusha) nayo pia ya serikali, iliyo na historia ya kuingia kumi bora kwa muda mrefu na Tandahimba (Mtwara), ambayo pia ni ya serikali. Zilizoshika mkia Shule zilizofanya vibaya ni Mpendae, Ben Bella na Tumekuja (Unguja), Green Bird Boys (Kilimanjaro), Jang’ombe na Kiembesamaki (Unguja), Tanzania Adventist (Arusha), Al-Ihsan Girls (Unguja), Azania (Dar es Salaam) na Lumumba ya Unguja.
*Vipanga sayansi
Watahiniwa waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi ni Hassan Gwaay (Tabora Boys), Mohamed Ally (Feza Boys), Joshua Zumba (Uwata); Ntahondi Ernest na Castory Munishi (Mzumbe), Zakaria Mwaipula ( Ilboru), Deogratias Mwanjmila (Mzumbe), Magreth Kakoko (Marian Girls), Bertha Nguyamu (St Mary’s Mazinde Juu) na Silaji Andrea (feza Boys).
*Wasichana/wavulana bora
Wasichana bora katika masomo ya sayansi ni Magreth (Marian Girls); Bertha Nguyamu, Mary Kilapilo na Regina Lugola (St Mary’s Mazinde Juu) na Nola Matolo (feza Girls).
Wengine ni Selina Pius (Pandahili), Queenlisajoan Olan’g (Marian Girls), Nasma Nyindo (Kilakala), Sheikha Rashid (Feza Girls) na Lilian Hema (Tabora Girls).
Wavulana ni Hassan (Tabora Boys), Mohamed (Feza Boys), Joshua Zumba (Uwata), Ntahondi Ernest na Castory Munishi (Mzumbe), Zakaria Mwaipula (Ilboru), Deogratias Mwanjmila ( Mzumbe), Silaji Andrea (Feza Boys), Said Saidi (Tabora Boys) na Enock Mwambeleko (Marian Boys).
*Vipanga biashara
Waliofanya vizuri katika masomo ya biashara ni Japhet Lawrance (Tusiime), Juliana Mwalupindi (Weruweru), Arnold James (Umbwe), Halima Kulava (Al-Muntazir), Fredrick Laizer (Jude), Davic Swai (St Joseph Cathedral), Albertina Mella (Kazima), Lucy Sanga (Alpha), James Albanus (Kibaha) na Mussa Ambika (St Joseph’s Cathedral).
Wasichana bora katika masomo ya biashara ni Juliana (WeruWeu), Halima Kulava (Al-Muntazir), Albertina (Kazima), Lucy Sanga(Alpha), Husna Mori (Loyola), Rahmat Mandara (St Mary Goreti), Sauda Kitalima (Weruweru), Happiness Kira (St Mary Goreti), Itika Mwakisambwe (Weruweru) na Radegunda Dionis (Kazima).
Wavulana ni Japhet (Tusiime), Arnold (Umbwe), Fredrick (Jude), Davic (St Joseph Cathedral), Albertina Mella (Kazima), James (Kibaha) na Mussa (St Joseph’s Cathedral), Twalib Ally (Tusiime), Yusufu Msangi (Kirinjiko), Daniel Awestone (Kibaha) na Suleiman Hamad (Chasasa).
*Vipanga lugha/sanaa
Waliofanya vizuri kwenye masomo ya lugha na sanaa ni Edith Msenga (St Mary’s Mazinde Juu), Boniphac Kajaba (Manow Lutheran Jnr Seminary), Elikana Simon (Runzewe), Emmanuel Msabi (Kisimiri) na Straton Ngowi (Uru Seminary).
Wengine ni Leonce Bizimana (Milambo), Emanuel Gewe (Mpwapwa), Zuhura Abdul (Feza Girls), Shamsi Salim (Ridhwaa Seminary) na Editha Mgina (Bigwa Sisters Seminary).
Wasichana bora katika masomo ya lugha na sanaa ni Edith (St Mary’s Mazinde Juu), Zuhura (Feza Girls), Editha (Bigwa Sisters Seminary), Vivian Magesa (Lake), Vaileth James (chief Ihunyo), Christina Mtangi na Asnath Masanza (St Mary’s Mazinde Juu) na Neema Paul (Tabora Girls).
Wengine ni Lohi Ako(Weruweru) na Edna Leonard (Loyola) wakati wavulana ni Boniphac ( Manow Lutheran Jnr. Seminary), Elikana (Runzewe), Emmanuel (Kisimiri), Straton (Uru Seminary), Leonce (Milambo), Emanuel (Mpwapwa), Shamsi (Ridhwaa Seminary), Mabula Makelemo(Winning Spiriti), Faraja Almas (Pandahill) na Paschal Alexander (Kisimiri).
Dk Msonde alisema baraza limezuia matokeo ya wanafunzi 10 wa shule waliopata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa baadhi ya masomo na wengine 36, waliopata matatizo ya kiafya walioshindwa kufanya mitihani yote ambao watapewa nafasi nyingine.
Aidha, baraza hilo limefuta matokeo ya watahiniwa 25 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani, kwa kuingia na vikaratasi vyenye maandishi na simu kwenye vyumba vya mitihani, kati ya hao watahiniwa 21 wakiwa ni wa shule na wanne wa kujitegemea.
Akizungumzia matokeo ya mtihani wa uwalimu, Msonde alisema watahiniwa 10,747 waliofanya mtihani Daraja A wamefaulu, wasichana wakiwa ni 5,065 na wavulana 5,682 wakati watahiniwa wa Stashahada ya Ualimu Sekondari 337 waliofanya mtihani huo wamefaulu, wasichana wakiwa 72 na wavulana 265.
“Baraza pia limefuta matokeo yote ya mtahiniwa mmoja aliyebainika kufanya udanganyifu katika mtihani wa Ualimu Daraja A,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment