Monday, 18 July 2016

RAIS MAGUFULI AIBUA UFISADI MWINGINE WA MABILIONI JESHI LA POLISI

Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.

Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi kujiepusha na vitendo vya rushwa vinavyolifanya jeshi hilo kukosa heshima katika jamii huku akifichua kuwepo kwa taarifa zinazolihusisha jeshi hilo na wizi wa mabilioni yaliyotolewa kwa ajili ya ununuzi wa sare za jeshi hilo mwaka 2015.

“Mnajua kupeleleza, mna vyombo vyote, ofisi ya IGP ipo palepale, makamishna wote mnazunguka, mnakwenda palepale, mwizi mnae palepale, mnashindwa kumshika,” alisema

Rais Magufuli ameyasema hayo leo alipokuwa akiwaapisha makamishna wa Jeshi la Polisi waliopandishwa vyeo hivi karibuni.

Ameliagiza jeshi hilo kuwaondoa watumishi wote wasiokuwa askari Polisi na ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa taratibu na ufujaji wa fedha za umma ili kulinda heshima, nidhamu na uadilifu ndani ya jeshi hilo.

“Kama mnafikiri kuwa na raia katika jeshi la Polisi wanawaharibia kazi zenu hamisheni rai wote wapelekeni utumishi, kwani hakuna mhasibu ambaye ni askari Polisi, hakuna mhandisi ambaye ni askari Polisi, hakuna afisa tawala ambaye ni askari Polisi?...mimi nafikiri kama matatizo ya wizi na wafanyakazi hewa yanaletwa na raia waliomo ndani ya jeshi la Polisi na majeshi yetu mengine, IGP kaorodheshe rai wote wanaofanya kazi ili waondolewe na tuwapangie kazi nyingine uraiani,” alisema.

Ameshangazwa na jeshi hilo kutoa kiasi cha fedha kinachokadiriwa kuwa kati ya Sh Bilioni 40 hadi 60 kwa ajili ya sare za polisi ambazo hadi leo hakuna hata moja iliyonunuliwa na wakati huohuo jeshi hilo likikosa shilingi bilioni 4 tu za kukomboa magari yao zaidi ya 70 yanayoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huko bandarini.

Aidha, Rais Magufuli ameagiza uchunguzi ufanyike na wahusika wafikishwe mbele ya haki kusudi hata nusu ya fedha hizo ziweze kurudishwa kusudi ikalipie magari ya polisi yaweze kutoka bandarini maramoja.


Amelitaka pia Jeshi la Polisi kuachana na utaratibu wa kuwa na watumishi ambao ni raia wa kawaida na badala yake polisi wenyewe ndio washike nafasi hizo kulingana na taaluma husika na kushangazwa na taarifa kuwa  Mhasibu Mkuu wa Polisi aliyetumbuliwa hivi karibuni kwa tuhuma za ubadhirifu alikuwa raia wa kawaida na sio polisi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment