Monday, 18 July 2016

MTANDAO WA MAI WAMUOMBA MAGUFULI AFUTE LESENI ZA BIASHARA


WADAU wa sekta ya biashara katika mikoa mitano iliyopo katika Ukanda wa Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) wamemuomba  Rais Dk John Magufuli kufuta leseni za biashara wakidai kwamba zimekuwa kizuizi cha uanzishaji wa biashara mpya hasa kwa wajasiriamali wadogo.

 Wadau hao waliounda mtandao unaotafiti kero za kibiashara (Multi Actors Integration-MAI) katika mikoa hiyo ya Iringa, Morogoro, Mbeya, Njombe na Ruvuma ili zifanyiwe kazi walisema kuondolewa kwa leseni kutasaidia kuijenga zaidi sekta binafsi na kuchangia pato kubwa zaidi serikalini.

“Utaratibu wa leseni umekuwa kero kwa wajasirimali wanaotaka kuanzisha biashara mpya kwasababu hawawezi kuzipata mpaka wawe na tax clearance ambayo hutolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania baada ya kukadiriwa na kulipa kodi,” alisema Mwenyekiti wa MAI, Lucas Mwakabungu.

Katika kikao chao kilichofanyika jijini Mbeya hivikaribuni kwa lengo la kupitia utekelezaji wa majukumu yao ya kipindi cha miezi sita iliyopita, Mwakabungu alisema watu wanapokuwa na fursa ya kuanzisha biashara halali bila kuwa na kikwazo chochote ni rahisi biasharaza zao zikarasimishwa na kuanza kulipiwa kodi.

Alimpongeza Rais kwa mikakati yake mbalimbali inayolenga kujenga uchumi unaokwenda kuboresha sekta binafsi lakini akaiomba serikali iangalie mzigo wa kodi zinazotozwa katika kila biashara na kuangalia namna ya kuzipunguza.

“Zipo baadhi ya biashara zinalipiwa kodi nyingi na hiyo ni kwasababu ya biashara hizo kuwa na mdhibiti zaidi ya mmoja,” alisema Mwakabungu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoa wa Iringa.

Kwa upande wake, Dk Goodluck Urassa wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Shule Kuu ya Biashara na Mratibu wa Mradi unaondeshwa pamoja na program ya BEST inayoshughulikia kuboresha mazingira ya biashara Tanzania alisema serikali inakila sababu ya kuboresha mazingira ya biashara ili yatanue wigo wa ajira nchini.

Alisema kwa kupitia program ya BEST mtandao wa MAI umeanza kuibua mambo mbalimbali yanayoongeza kero kwa wafanyabiashara na kufanya utetezi.

“Tunashughulikia mambo ya kodi za mazao, vipimo, bidhaa feki, pembejeo feki. Tunafanya utafiti, tunatoa mafunzo na tunatoa ushauri na kufanya mazungumzo na serikali ili kuiboresha sekta hii ya biashara,” alisema.

Akitoa mfano wa tafiti zilizofanywa kwa kupitia program ya BEST, Dk Urassa alisema; “mwaka 2012 tulifanya utafiti wa vipimo vya mahindi na mpunga na kubaini serikali na wakulima wenyewe wanapoteza fedha nyingi kwasababu ya ujazo wa ziada maarufu kama lumbesa.”

Alisema utafiti wao kuhusu vipimo vya Lumbesa unaonesha serikali imekuwa ikipoteza zaidi ya Sh Bilioni 14.8 kama mapato ya kodi huku wakulima nchini kote wakipata hasara ya zaidi ya Sh Bilioni 174 kila mwaka.

Kuhusu matumizi ya pembejeo feki alisema utafiti wao walioufunya mkoani Njombe na unaonesha zimekuwa zikipenya hadi kwa wakulima kwa njia mbalimbali ikiwemo ya matumizi ya lebo feki, upakaji wa rangi inayofanana na pembejeo halisi katika pembejeo feki na kwasababu ya kuendelea kutoa vibali za usambazaji wa pembejeo kwa watu au kampuni zinazokosa sifa ya uaminifu.

Pamoja na mikoa hiyo mitano inayowakilishwa na chemba zao za TCCIA, taasisi zingine zilizopo katika mtandao huo wa MAI ni pamoja na Umoja wa Vyuo Vikuu Nchini, vyombo vya habari na washirika wengine katika sekta ya biashara na kilimo likiwemo Jukwaa la Wadau wa Kilimo Tanzania (ANSAF), taasisi inayojihusisha na kilimo cha mbogamboga, matunda na maua nchini (TAHA) na mpango wa SAGCOT wenyewe.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment