Wednesday, 20 July 2016

MAUAJI YA DAUDI MWANGOSI KUTOLEWA HUKUMU KESHO


HUKUMU ya kesi ya mauaji ya mwanahabari Daudi Mwangosi inayomkabili askari Polisi Pacificius Cleophace Simoni, itatolewa kesho Julai 21, mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, ilipokuwa ikisikilizwa.

Hukumu hiyo itatolewa na Jaji Paulo Kiwehlo ambaye hivikaribuni aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Kwa mara ya kwanza Simoni alifikishwa mahakamani hapo Septemba 12, 2012 akituhumiwa kumuua Mwangosi kwa kukusudia katika tukio lilitokea katika kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi Mkoani Iringa Septemba 2, 2012 wakati mwandishi huyo alipokuwa akiwajibika katika kazi zake za kutafuta habari wakati wa ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Juni 23, mwaka huu mtuhumiwa huyo alijitetea mbele ya mahakama hiyo akisema hamfahamu wala hakuwahi kumuona marehemu Mwangosi.

Akiongozwa na wakili wake, Lwezaula Kaijage wakati akitoa utetezi wake, mtuhumiwa huyo alikana ungamo lake alilosaini Septemba 5, 2012 kwa Mlinzi wa Amani Frola Mhelela akikiri kumuua Mwangosi na kuwajeruhi askari wengine wanne baada ya kufyatua bomu kutoka katika silaha aliyokuwa akitumia.

Alikana ungamo hilo akidai alilisaini bila kujua lina maelezo gani na yenye lengo gani kwa kupitia amri iliyotolewa kijeshi na aliyekuwa Afisa Upelelezi wa Mkoa wa Iringa (RCO), Nyigesa Wankyo.

Simoni aliikana pia picha iliyochapishwa ukurasa wa mbele wa gazeti la Mwananchi la Septemba 3, 2012 ikumuonesha akiwa amemuelekezea marehemu Mwangosi silaha inayotumika kupiga mabomu ya mchozi na ya kishindo, akisema sio yeye.

Pamoja na kwamba alitumia mabomu sita (matatu ya kishindo na matatu ya machozi) kwa kupitia silaha hiyo, alisema aliirudisha katika ghala la kuhifadhia silaha mjini Iringa ikiwa katika hali nzuri; tafsiri aliyosema kwa kijeshi ina maana haikuleta madhara yoyote katika eneo la tukio.

Wazee wawili kati ya watatu wa baraza la wazee wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa walisema Polisi Pacificius Cleophace Simoni anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya mwanahabari Daudi Mwangosi; alimuua mwanahabari huyo kwa kuzingatia maelezo yake ya ungamo aliyoyatoa kwa Mlinzi wa Amani Septemba 5, 2012.


Wakati upande wa utetezi katika kesi hiyo uliwakilishwa na wakili Lwezaula kaijage, upande wa Jamuhuri (mashitaka) uliwakilishwa na mawakili wawili,  Ladslaus Komanya na  Sandy Hyra.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment