Sunday, 31 July 2016

LOWASSA AFUNGUKA AKISEMA HAKUNA MWENYE HATI MILIKI YA NCHI HII


Aliyekuwa Mgombea Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa amedai kuwa hakuna mtu mwenye hati miliki ya nchi hii wakati akimtaka Rais wa Jamuhuri ya Muungano, Dk John Magufuli kuwa na utamaduni wa kufanya mazungumzo na wanasiasa wenzake ili kutafuta muafaka mambo mbalimbali ya kisiasa nchini.

Akihojiwa na Tido Mhando wa Televisheni ya Azam kupitia kipindi cha Funguka, Lowassa amesema siasa ni mazungumzo na sio kutoa amri za kiimla kama anavyofanya Magufuli.

Amesema ni dhuluma na ni kinyume kisheria na kikatiba kuwazuia watanzania kufanya  siasa hadi mwaka 2020 kama inavyoelekezwa na Rais Magufuli.

Akitetea uamuzi wa CHADEMA uliokuja na operesheni ‘Ukuta’ hapo Septemba 1, mwaka huu, Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu msaatfu alisema oparesheni hiyo ni sahihi kabisa.

Pamoja na usahihi wake alisema bado kuna nafasi ya kufanya mazungumzo kabla ya tarehe hiyo ili kuepusha hali ya migogoro itakayojitokeza siku hiyo kwa manufaa ya pande zote.

Akizungumzia barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukemea operesheni hiyo, amesema barua hiyo imejaa ghadhabu zaidi kuliko kuongelea mambo ya msingi ambayo vyama vya upinzani vimekuwa vikionewa.

Akiongelea suala la wabunge wa upinzani kutoka na kususia bunge, Lowassa amesema hali hiyo ilisababishwa na kutokuwepo kwa Spika Job Ndugai ambaye kwa muda mrefu alikuwa nje ya nchi akiendelea na matibabu.

“Ndugai angekuwepo haya yote yasingetokea kwakuwa ni mtu makini sana. Kwa Naibu Spika kuna tatizo la Kisaikolojia kwasababu aliingia bungeni kwa njia zisizoeleweka na hivyo kumfanya kushindwa kuhimili kiti hicho vizuri,” amesema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment