Tuesday, 5 July 2016

KASESELA AZUIA MIKUTANO YA WANASIASA WILAYANI KWAKE
MKUU wa Wilaya Iringa, Richard Kasesela amesema kamati yake ya ulinzi na usalama haitaruhusu mikutano ya hadhara itakayoombwa na vyama vya siasa wilayani humo ili kuipa serikali na wananchi nafasi ya kujiletea maendeleo baada ya kumaliza salama Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Pamoja na uamuzi huo, Kasesela amesema kamati hiyo itawasaka na kuwafikisha katika vyombo vya dola watu wanaomkashifu Rais Dk John Magufuli na viongozi wengine wa serikali, siasa na dini kwa namna yoyote ile.

“Tuendelee na majukwa ya utendaji, majukwaa ya mipasho ya siasa tupumzike ili tuiache serikali ifanye kazi zake,” alisema baada ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza kuwaapisha wakuu wa wilaya za mkoa wa Iringa mapema jana.

Kasesela alisema uchaguzi wa 2015 ulimalizika salama kwa kumpata rais, wabunge na madiwani na kwamba kazi inayofanywa na Rais kwasasa ni kumalizia kuunda serikali yake.

“Kama tunataka mbwembwe za siasa majukwani aidha tusubiri uchaguzi wa serikali za mitaa au Uchaguzi Mkuu wa 2020,” alisema huku akivitangazia vyama vya siasa ruksa ya kufanya mikutano yao ya ndani akiahidi hawataiingilia kama itafanyika kwa amani.

Wakati huo huo, Kasesela amewataka viongozi wa taasisi mbalimbali za dini ambazo hakuzitaja kumaliza migogoro yao ya uongozi aliyosema inaelekea kuhatarisha amani ya wilaya.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdala ameahidi kuzishughulikia changamoto mbalimbali za kimaendeleo wilayani humo kwa misingi ya haki na kwa kuzingatia sheria na maagizo ya viongozi wake wakuu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Jamuhuri William ameahidi kuifanya wilaya ya Mufindi ya mfano katika elimu na huduma nyingine za kijamii katika kipindi chote atakachokuwa kiongozi wake.

Baada ya kuwaapisha wakuu hao wa wilaya, Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliwataka wahakikishe wanakamilimisha ujenzi wa madarasa, maabara, vyoo bora, majengo ya utawala na nyumba za walimu baada ya zoezi la utengenezaji wa madawati kufanikiwa kwa asilimia 100.

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa chakula, Masenza aliwataka wawasimamie wananchi ili kila mmoja awe na chakula cha kutosha akisema ni aibu kwa mkoa huo wenye ardhi yenye rutuba kuwa na kaya zinazokumbwa na njaa na kuomba chakula.

Aidha aliwataka wakuu hao wa wilaya kuhakikisha wafanyabiashara wanatoa risiti za EFD kila wanaptoa huduma kwa wananchi, kuzisaidia halmashauri zibuni vyanzo vipya vya ukusanyaji wa mapato, kushughulikia migogoro ya ardhi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Maagizo mengine ni pamoja na kukabiliana na tatizo la utapiamlo na udumavu, kuhakikisha vijana wanafanya kazi, wananchi wanajiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF), kupambana na uhalifu na kuimarisha utawala bora.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment