Sunday, 17 July 2016

KAMATI YA VIBALI VYA UVUNAJI MITI YASHAMBULIWA

WADAU wa sekta ya biashara ya mazao ya miti nchini, wameishambulia kamati ya kitaifa ya ushauri wa ugawaji wa vibali vya uvunaji wa miti ya mbao katika mashamba ya serikali wakiifananisha na magugu maji yanayochochea migogoro ya upataji wa vibali hivyo.

Wadau hao, wakiwemo wavunaji wenye viwanda vya mbao wa wilayani Mufindi Mkoani Iringa walisema kamati hiyo haileweki kwa wadau, wapi inapata taarifa na ushauri inaotoa kwa waziri mwenye dhamana ili kumaliza migogoro katika sekta hiyo inayozidi kukumbwa na upungufu wa malighafi hiyo mashambani.  

Hivikaribuni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kusitisha utoaji wa vibali vya uvunaji wa miti katika mashamba ya serikali nane ya miti ya kupandwa yanayosimamiwa likiwemo shamba kubwa kuliko yote nchini la Saohill lililopo wilayani Mufindi.

Lawama hizo wamezitoa juzi wakati Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) kwa ufadhili wa shirika la BEST-AC lilipokuwa likizindua utafiti unaolenga kujua changamoto za kiutawala katika utoaji wa vibali vya uvunaji miti kibiashara katika misitu ya serikali.

Utafiti huo ulioanza kutekelezwa hivikaribuni kupitia wataalamu washauri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Reuben Mwamakimbullah, Stephano Kingazi na Mboka Mwanilu utafanywa kwa wiki saba kupitia mradi wa miezi sita unaohusu mfumo wa ugawaji wa vibali katika shamba la miti la Saohill, Mufindi.

Akielezea kinachotarajiwa katika utafiti huo, Kingazi alisema utasaidia kutafuta mfumo madhubuti wa ugawaji rasilimali na vibali vya uvunaji katika shamba hilo na mashamba mengine ya serikali nchini yanayotoa vibali vya uvunaji na kuwasilishwa serikalini.

Mwenyekiti wa Chama cha Wavunaji wenye Viwanda vya Mbao katika Msitu wa Saohill Mufindi (SAFIA), Henry Lukambinga alisema; “wavunaji walioko katika msitu wa Saohill hawazidi 300 lakini inashangaza kuona wanaopata vibali kila mwaka ni zaidi ya 800.”


Lukambinga alisema wenye viwanda wamekuwa wahanga wakubwa wa maamuzi ya ugawaji wa vibali hivyo kwani wamekuwa wakipata migao midogo ya uvunaji wakati mwingine kikiwa sawa na wasio na viwanda wala mashine za kupasua mbao.

“Tumeweka mitaji mikubwa katika sekta hii. Tumetumia fedha nyingi kununua mashine za kisasa kwa ajili ya upasuaji mbao, chakushangaza kila mwaka malighafi inapungua kwasababu wengi wanaopata hawana sifa,” alisema.

Alisema kiwanda chake kilichopo Kinyanambo Mafinga kina uwezo wa kuchakata mita za ujazo 100,000 za magogo kwa mwaka lakini toka kianzishwe hakijawahi kupata hata nusu ya kiasi hicho cha magogo.

Alisema migogoro ya vibali itakwisha kama serikali itazingatia taratibu, kanuni na sheria bila kusahau sifa zote muhimu anazotakiwa kuwa nazo mvunaji anayestahili kupata kibali.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wavunaji Miti katika Shamba la Saohil (UWASA), Carlos Kinyoa alisema wakati kukiwepo na taarifa ya uwepo wa kamati ya kitaifa ya ushauri wa utoaji wa vibali hivyo, wengi wa watu wanaopata vibali vya uvunaji ni wale ambao hawajui hata lilipo shamba la Saohill au mashamba mengine ya misitu nchini.

“Hao ni ndugu, jamaa na marafiki wa baadhi ya viongozi wa idara mbalimbali za serikali nchini wanaopata vibali kupitia vimemo vya viongozi hao ili wauze kwa wavunaji wenye sifa jambo linalofanya bei za mazao ya miti zikiwemo mbao ziendelee kupanda siku hadi siku,” alisema.

Katibu wa SAFIA, Oscar Kaduma aliishambulia kamati hiyo akisema kwanini isiitwe magugu maji kama haijakita mizizi yake mpaka kwa wadau wa sekta hiyo.

“Tunahitaji kupata wavunaji sahihi watakatambuliwa kwa viwanda na mashine zao kama sheria, kanuni na taratibu zinavyotaka ili kuondoa utoaji wa vibali kwa watu wasio na viwanda na mashine,” alisema.

Akikosoa misingi ya usimamizi endelevu wa misitu nchini, Mshauri Elekezi Kingazi alisema Sheria ya Misitu Na 14 ya mwaka 2002 inatambua mpango wa usimamizi bila kutaja mpango wa matumizi ya misitu.

“Sheria haijatoa tafisri ya viwanda vya misitu wala haitaji biashara ya ndani ya mazao ya misitu,” alisema.

Akizungumzia changamoto ya utoaji wa vibali vya uvunaji, Meneja wa Msitu wa Saohill Saleh Beleko alisema changamoto hiyo ni kubwa kwasababu mahitaji na wahitaji ni wengi lakini inaweza kumalizwa kwa kutumia mfumo wa uuzaji wa miti hiyo kwa njia ya mnada.


“Au kuwepo na kampuni itakayokuwa inapewa tenda ya uvunaji ili wenye viwanda wakanunue huko vinginevyo ni lazima kuwe na mfumo utakaozingatia maslai ya pande zote kwasababu rasilimali hii ni mali ya watanzania wote,” alisema.

Reactions:

1 comments:

  1. hahahaha msitu wa watanzania wote sio wa wenye viwanda Magufuri haki ni ya wana iringa wote na watanzania w anaofata sheria

    ReplyDelete