Thursday, 21 July 2016

HUKUMU KESI YA MAUAJI YA MWANGOSI YAPIGWA KALENDA HADI JUMATATU


HUKUMU ya kesi ya mauaji ya mwanahabari Daudi Mwangosi iliyokuwa itolewe leo, Julai 21, 2016 imeahirishwa hadi Jumatatu Julai 25.

Kesi hiyo inayomkabili askari Polisi Pacificius Cleophace Simoni ambaye hivi karibuni alijitetea kwa kupinga kuhusika na mauaji hayo.

Akiahirisha hukumu ya kesi hiyo, Kaimu Msajili wa Mahakama hiyo, Jofrey Isaya alisema inaahirishwa kwasababu Jaji Paulo Kiwehlo aliyekuwa akiisikiliza yuko nje ya Iringa kwa majukumu mengine ya kikazi.

Kabla ya kuanza kwa shughuli za kimahakama, hofu ilitanda kwa wanahabari na watu wengine waliojitokeza kwa wingi kusikiliza hukumu hiyo kutokana na idadi kubwa ya askari Polisi, wenye sare na wasio na sare, waliokuwepo nje na ndani ya viunga vya mahakama hiyo.

Katika hali isiyo ya kawaida, kila aliyekuwa akiingia ndani ya viunga vya mahakama hiyo kwa kupitia lango kuu alikuwa akigaguliwa na Polisi hao walioondoka mara tu baada ya hukumu ya kesi hiyo kuahirishwa.

Pamoja na askari hao kulikuwepo na magari ya Polisi, yakiwemo mawili aina ya Landlover Defender ambayo mojawapo hutumika kumleta mtuhumiwa huyo tofauti na gari linalotumiwa kuwaleta watuhumiwa wengine wa kesi mbalimbali mahakamani hapo.

Chumba cha mahakama kilichotumika kuahirisha kesi hiyo kilikuwa na askari zaidi ya 20, wakiwemo waliobeba silaha kali za moto hali iliyokuwa ikitishia utendaji kazi wa baadhi ya wanahabari ambao mara kwa mara wamekuwa wakizuiwa na askari hao kupiga picha kabla ya kuanza kwa shughuli ya mahakama.

Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deo Nsokolo aliunga na wanahabari zaidi ya 20 wa mjini Iringa na kushuhudia jinsi wanahabari wanavyopata misukusuko wakati wa kuripoti kesi hiyo.

“Nimekuja mjini Iringa kuuungana na wanahabari wa mkoa wa Iringa na kuwawakilisha wanahari nchini kote kusikiliza hukumu ya kesi hii ambayo ni muhimu sana kwa tasnia ya habari hapa nchini,” alisema.

Kaimu Msemaji wa Mahakama hiyo, Lusako Mwang’onda alisema mahakama hiyo itahakikisha wanahabari wanapata haki yao ya kimsingi ya kupata habari wawapo mahakamani.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Peter Kakamba hakuweza kupatikana ili atoe ufafanuzi wa yale yanayojitokeza mahakamani kila mtuhumiwa huyo anapofikishwa mahakamani hapo.

Kwa mara ya kwanza Simoni alifikishwa mahakamani hapo Septemba 12, 2012 akituhumiwa kumuua Mwangosi kwa kukusudia katika tukio lilitokea katika kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi Mkoani Iringa Septemba 2, 2012 wakati mwandishi huyo alipokuwa akiwajibika katika kazi zake za kutafuta habari wakati wa ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Reactions:

0 comments:

Post a Comment