Monday, 18 July 2016

CCM IRINGA YATUMIA ZAIDI YA SH MILIONI 350 KUKARABATI UWANJA WAKECHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa kimetumia zaidi ya Sh Milioni 350 kuufanyia ukarabati uwanja wake wa michezo wa mjini Iringa wa Kumbukumbu ya Samora.

Akizungumza na wanahabari uwanjani hapo jana, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Hassan Mtenga alisema pamoja na kukarabati mandhari ya uwanja huo, kiasi hicho cha fedha kimetumika kukarabati sehemu inayotumika kuchezea mpira wa miguu (Pitch).

Mtenga alisema fedha hizo zimechangwa na wadau mbalimbali wenye mapenzi mema na chama hicho na maendeleo ya michezo hasa wa mpira wa miguu mkoani Iringa huku akilalamika hatua ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutochangia chochote katika ukarabati huo unaozinufaisha pia timu wanachama wake.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa ambaye pia ni Rais wa Lipuli FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza , Jesca Msambatavangu alisema; “mchakato wa ukarabati wa uwanja huo ulianza mwaka jana kwa kukarabati kuta na sehemu za kukalia watazamaji  na baadaye tulifumua sehemu ya katikati ambayo inatumika kuchezea soka.”

Alisema eneo la kuchezea mpira wa miguu limechelewa kukamilika baada ya kubainika kuwepo kwa mchwa waliosababisha nyasi zisiote vizuri na vichuguu..

“Baada ya kubaini tatizo hilo tulilazimika kuanza upya kazi ya kutengeneza kiwanja hicho cha mpira wa miguu kwa kuwadhibiti mchwa hao,”alisema.

Alisema uwanja huo utakuwa umekamilika katika kipindi cha siku 21 zijazo na kwamba baada ya hapo utakuwa tayari kwa matumizi ya mpira wa miguu na shughuli zingine za michezo.

Kuhusu maandalizi ya Lipuli FC katika ligi hiyo inayotarajiwa kuanza baadaye mwaka huu, Msambatavangu alisema tayari wamekwishasajili wachezaji wapya 10 watakaoungana na wachezaji waliobakishwa kutoka kikosi cha timu iliyopita.


Aliwaomba wadau wa maendeleo wa mkoa wa Iringa kujitokeza kwa wingi kuiwezesha timu hiyo ili katika mikakati yao waliyojiwekea iweze kupanda hadi Ligi Kuu ya msimu ujao.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment