Wednesday, 27 July 2016

BREAKING NEWS , ASKARI ALIYEMUUA MWANAHABARI MWANGOSI AFUNGWA JELA MIAKA 15


MAHAKAMA  kuu ya Tanzania  kanda  ya  Iringa  leo  imemuhukumu kwenda  jela miaka  15 askari wa kikosi cha  kutuliza ghasia (FFU) mwenye  namba G .2573 Pacificius Cleophace Simon (27)  aliyekutwa na hatia ya kumuua bila kukusudia mwandishi  wa  habari  wa  kituo  cha Chanel Ten Daudi  Mwangosi.


Akitoa hukumu hiyo, Jaji Dk Paulo Kiwehlo amesema mahakama ni mahali pa sheria na wala si pa kusikiliza maoni ya watu .

Simoni alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Septemba 12, 2012 akituhumiwa kumuua Mwangosi kwa kukusudia katika tukio lilitokea katika kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi Mkoani Iringa wakati mwandishi huyo alipokuwa akiwajibika katika kazi zake za kutafuta habari wakati wa ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mapungufu ya ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamuhuri uliilazimisha Mahakama Kuu Kanda ya Iringa chini ya jaji huyo kulibadili shauri hilo kutoka kwenye kesi ya mauaji ya kukusudia na kuwa ya mauaji ya bila kukusudia. 


Akitoa hukumu hiyo iliyomchukua takribani dakika 22 kuisoma jana, Jaji Dk Kiwehlo alisema pamoja na miaka minne aliyokaa mahabusu mara baada ya kutuhumiwa na hatia hiyo; “haki itatendeka iwapo mtuhumiwa atakwenda jela miaka mingine 15, hiyo ni kwa kuzingatia ukubwa wa kosa ambalo amekutwa nalo mahakamani.”

Alisema lengo la kutoa adhabu ni kufikia mizania ya kosa lililotendwa kwa kuzingatia maelezo na maombi ya upande wa utetezi na ule wa mashtaka ambayo yana mgongano wa hisia na maslai.

Alisema wakati upande wa utetezi uliiomba mahakama hiyo imuachie mtuhumiwa huyo kwa masharti kwa mujibu wa kifungu cha 38 (11) cha sheria ya kanuni ya adhabu, upande wa Jamuhuri uliomba afungwe maisha kwa mujibu wa kifungu cga 198 cha sheria ya kanuniya adhabu.

“Pamoja na hayo mahakama inafahamu kwamba adhabu hutolewa  kama sehemu ya onyo kwa mtuhumiwa na sio kama kisasi hiyo ni kwa lengo la kusaidia kuzuia mambo kama hayo yasiendelee kutokea katika jamii,” alisema.

Jaji Dk Kiwehlo alisema hakuafikiana na ombi la utetezi la kumuachia mutuhumiwa kwa masharti maalumu kwasababu msingi wa adhabu unatakiwa ufanane na kosa lililofanywa na muhusika anayetiwa hatiani.

Alisema mahakama haitakuwa na busara na ingepoteza imani na kuonekana kwa wananchi kama chombo kisichotenda haki endapo ingemuachia mtuhumiwa huyo kwa masharti. 


“Na sikukubaliani na ombi la upande wa Jamuhuri la kumfunga maisha kwasababu haitasaidia kumrekebisha kwa kuzingatia misingi ya utoaji wa adhabu,” alisema.

Pamoja na mahakama kutambua ukubwa wa kosa lililofanywa na mtuhumiwa huyo na madhara waliyoyapata katika familia ya marehemu  alisema mahakama imemfikiria kwa kumpa adhabu nyingine ambayo ni ya miaka 15 jela.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo, mke wa marehemu, Itika Mwangosi alisema; “kwanza kabisa napenda kutanguliza shukrani kwa Mungu aliyetupigania na kutulinda mpaka siku hii ya hukumu. Pili nawashukuru wanahabari kwa kazi kubwa ya kuhabarisha umma kuhusu kesi hii.”

Pamoja na kifo kilichomkuta mumewe wakati akitekeleza wajibu wake, aliwatia moyo wanahabari akiwataka wasiogope vikwazo vya dola, wasonge mbele katika kazi zao za kuhabarisha umma kwakuwa bila wao jamii haiwezi kujua kinachoendelea.

Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deo Nsokolo alisema; ‘Tunaishukuru mahakama kwa maamuzi hayo kwasababu kulikuwa na dalili ya upande wa mashtaka wa kuharibu kesi hiyo.”

Akitoa ufafanuzi wa namna kesi hiyo ilivyoharibiwa, Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), Tukusiwga Mwaisumbe alisema kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo kukiwa hakuna shahidi hata mmoja kutoka katika makundi mengine muhimu wakiwemo wanahabari, wananchi na viongozi wa Chadema waliokuwepo katika tukio.

Swiga alisema pamoja na mashahidi hao kutoitwa mahakamani, upande wa Jamuhuri ulishindwa kumuita mwanahabari aliyepiga picha iliyochapishwa katika vyombo mbalimbali vya habari ikionesha jinsi mauaji hayo yalivyofanyika na kuwaita viongozi mbalimbali wa jeshi la Polisi waliokuwepo katika tukio hilo la mauaji akiwemo aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda .

Katika kesi hiyo upande wa Jamuhuri ulikuwa na mashahidi wanne, ambao kati yao watatu walikuwa askari Polisi na mmoja alikuwa mlinzi wa amani ambaye ushahidi wake ndio uliosaidia kumtia hatiani mtuhumiwa huyo.

Rais wa UTPC alisema tukio hilo na mwenendo wake vimeiingiza Tanzania katika rekodi yenye mashaka ya namna jeshi la Polisi linavyofanya kazi na wadau wake wakiwemo wanahabari.

Nsokolo alisema baada ya kupokea nakala ya hukumu ya kesi hiyo UTPC kwa kushirikiana na wadau wengine likiwemo Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), watahakikisha wanashirikiana na familia ya marehemu hiyo iweze kulipwa fidia kwa kumpoteza ndugu yao aliyekumuwa muhimili wa familia.

Makamu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile alisema wanahabari wanaishukuru mahakama kwa maamuzi yake kwasababu mwenendo mzima wa kesi hadi hukumu hiyo inatolewa umethibitisha kwamba ipo huru.

“Pamoja na ushaidi dhaifu uliowasilishwa na Jamuhuri, mahakama imeamua kutenda haki kwa kutumia ushahidi pekee wa mlinzi wa amani ambaye kama asingewasilisha ushahidi wake mahakamani hapo, kesi hiyo isingekuwepo,” alisema.

Alisema wakati wakijipanga kwa mchakato wa kupigania haki ya familia ya kupata fidia wataangalia kama kesi hiyo ifunguliwe katika mahakama ya Afrika au mahakama za ndani.

“Tutakaa na wenzetu ili tujue ni mkondo gani tutachukua kudai fidia, kama ni mahakama za ndani au ya nje ili iende kasi. Tunaomba familia ya Mwangosi itusaidie isimame na sisi,” alisema Balile.

Akizungumzia hukumu hiyo, Wakili wa utetezi, Lwezaula Kaijage alisema ni mapema mno kuzungumzia hatua atakayochukua baada ya hukumu hiyo.

“Kesi sio ya kwangu ni ya mshtakiwa, mimi nilikuwa na mtetea tu, nikishapata hukumu itabidi nikutane naye, nisikie maoni yake, niangalie sheria, mwenendo wa shauri, niangalie ni kitu gani ambacho mahakama ilijielekeza vibaya katika kufiakia uamuzi huo na kama itaonekana kipo tutaangalia hatua za kuchukua,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment