Tuesday, 19 July 2016

AIRTEL YATOA MSAADA WA VIFAA VYA USAFI DAR


KAMPUNI ya simu za mkononi ya Airtel imetoa msaada wa mapipa 15  ya kukusanya na kutunzia takataka  kwa serikali ya mtaa wa kumbukumbu   kata ya kinondoni mkoani dare s salaam.

Msaada huo una thamani shilingi milioni 3  umetolewa leo.
Aidha kampuni hiyo imeahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika shughuli mbalimbali za kutunza mazingira ili kuiwezesha jamii kuishi katika mazingira bora yatakayopelekea kuwa na afya bora.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano Ofisa mazingira wa Airtel , Ncheye Mazoya alisema: “Airtel tunatambua sana jitihada zinazofanywa na serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania  katika kutunza na kuweka mazingira ya jamii kuwa safi. kwetu sisi Airtel Tunaamini  kwamba  ili tuweze kufanya biashara lazima tuwe na mazingira safi na wateja wenye afya bora, na ndio maana leo hii tunaunga mkono harakati za serikali za kuhakikisha swala hili la kufanya usafi kila mahali linaendelea kufanikiwa.

Alisema kwamba  mapipa waliyoyatoa yatasaidia jamii ya kinondoni kuweka mazingira katika hali ya usafi na kusaidia kuepusha magonjwa ya milipuko ambayo yamekuwa ni changamoto kubwa sana nchini.

Kwa upande wake Katibu tarafa wa Kinondoni Fortunatus Fulgence Isakafu alishukuru na kuwapongeza Airtel kwa mchango wao na kuongeza kwamba tarafa yake ina mpango  mkakati wa kutekeleza kwa vitendo kampeni ya usafi kwa kuhamasisha jamii kujitolea katika kutunza mazingira yanayowazunguka na kuyaweka kuwa safi wakati wote.

“Airtel msaada wenu umekuja wakati sahihi kwa kuwa zoezi la usafi kwetu sisi ni endelevu, mapipa haya ya kuhifadhi taka yatasaidia sana kupunguza kuzagaa kwa taka kila mahali  na kurahisisha ukusanyaji taka kwa ajili ya kuzipeleka sehemu maalum kwa uteketezaji”


Reactions:

0 comments:

Post a Comment