Tuesday, 14 June 2016

Yanga kuzawadiwa mamilioni Agosti

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga na timu nyingine zilizoshiriki katika msimu ulioisha wa 2015/2016, zitakabidhiwa zawadi zao mapema mwezi ujao kutoka kwa Vodacom Tanzania.
Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu alisema kuwa ucheleweshaji wa kutoa zawadi hizo, umetokana na baadhi ya timu kushiriki mechi za mashindano ya kimataifa kama vile mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika na kuingia kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
“Tunaomba radhi kwa timu husika, wachezaji na wadau wa soka kwa zoezi hili kuchelewa ila tunawahakikishia kuwa zawadi ziko tayari na zitakabidhiwa mwezi ujao,” alisema Nkurlu. Pia alishukuru wadau wote waliofanikisha ligi hiyo hadi kufikia mwisho ambapo Yanga ya jijini Dar es Salaam iliibuka tena bingwa kwa mwaka huu.
“Licha ya changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ligi yapo mafanikio makubwa na ligi hii inazidi kuwa na msisimko mkubwa nchini tunawashukuru wadau wote na tuna imani kuwa itazidi kuwa bora katika siku za usoni,” alisisitiza Nkurlu.
Alisema kuwa Vodacom Tanzania itaendelea kutoa udhamini wa ligi hii hata katika msimu ujao kwa mujibu wa mkataba wake na TFF na aliwataka wadhamini wengine kujitokeza ili kuboresha zaidi ligi hii ikiwemo kuwawezesha wachezaji kunufaika zaidi katika ushiriki wake.
Vodacom ambayo imekuwa ikidhamini ligi hiyo kwa muda mrefu itatoa zawadi kwa mshindi wa kwanza, wa pili na wa tatu pamoja na kipa bora, mfungaji bora, kocha bora na wengineo.
Bingwa Yanga itaondoka na kitita cha Sh milioni 81, huku Azam FC iliyomaliza ya pili itapewa Sh milioni 40.6 wakati Simba iliyomaliza ya tatu itapewa Sh milioni 29 na Prisons ya Mbeya ina uhakika wa kupata milioni 23.3 baada ya kumaliza ya nne.
Kwa mujibu wa Lucas, timu yenye nidhamu itajipatia Sh milioni 17.9 huku kocha bora na mwamuzi bora kila mmoja atapewa Sh milioni 8.6, wakati Amis Tambwe wa Yanga atapata Sh milioni 5.7 baada ya kuibuka mfungaji bora wa ligi hiyo. Alifunga mabao 21. Mchezaji bora na kipa bora, ambao bado hawajajulikana kila mmoja atapewa kiasi cha Sh milioni 5.7 sawa na Tambwe.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment