Friday, 10 June 2016

Yanga kuingia kambini leo

TIMU ya soka ya Yanga inatarajiwa kuingia kambini leo kujiandaa na michezo ya hatua ya makundi itakayoanza kutimua vumbi Juni 17 mwaka huu. Yanga inatarajia kuanza mchezo wake wa kwanza ugenini mwishoni mwa wiki ijayo kwa kucheza na Moulodia Olympique Bejaia ya Algeria.
Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Yanga Hafidh Salehe alisema wataweka kambi Dar es Salaam na kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa kwa ajili ya maandalizi ya safari hiyo.
“Kesho (leo) tutaingia kambini Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kujiimarisha na kuhakikisha tunajiweka sawa kwa mazoezi tayari kwa mchezo wetu wa kwanza utakaochezwa,” alisema.
Kwa mujibu wa Salehe, wachezaji wote waliosajiliwa na wale wa zamani wataungana katika maandalizi hayo. Yanga tayari imesajili wachezaji wanne ambao ni Ramadhan Kessy, Juma Mahadhi, Andrew Vicent na kipa Ben Kakolanya.
Meneja huyo alisema wachezaji wote wapo isipokuwa Vicent Bossou ambaye anatarajiwa kuwasili wakati wote akitokea kwao Togo alikokuwa akitumikia timu yake ya Taifa. Alisema maandalizi yao yanaenda vizuri na kwamba uchaguzi unaoendelea Yanga hauwezi kuathiri mipango yao ya kujiandaa kwenda kuwakilisha vyema katika michuano hiyo. Yanga ilitinga hatua ya makundi baada ya kuifunga Esperanca ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment