Saturday, 18 June 2016

Waziri aeleza ugumu usambazaji sukari


Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwezeshaji, Charles Mwijage
SERIKALI imesema licha ya kuingiza nchini tani 41,000 za sukari usambazaji wake umekuwa wa kusuasua kutokana na kukosekana kwa ushirikiano kati ya wakuu wa mikoa na wasambazaji.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya sukari nchini.
Alisema serikali imefanya jitihada katika kuagiza sukari lakini usambazaji umekuwa wa kusuasua na kusababisha baadhi ya maeneo kuwa na upungufu.
Mwijage alisema hesabu za wataalamu kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani zinahitajika tani 40,000 kwa mwezi na hadi kufikia Juni 13 mwaka huu tayari tani 41,000 zilikuwa zimewasili bandarini, lakini changamoto kubwa imeonekana kuwepo kwenye usambazaji wa bidhaa hiyo.
Sambamba na hilo, wakuu wa mikoa na wilaya wameagizwa kuwasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Florens Turuka ili kuwasilisha mahitaji ya sukari kwenye maeneo yao. Alisema sukari ipo lakini tatizo lipo kwenye usambazaji unaosababishwa na ukosefu wa ushirikiano.
“Tulishasema sukari ipelekwe kila mkoa kwa ujazo mkubwa kuanzia tani 300-500 ili kudhibiti uhaba wa sukari, tukiwauliza wenye sukari wanasema sukari ipo lakini ukiwauliza wanunuzi wanasema sukari hakuna,” alisema Mwijage.
Hata hivyo alisema wizara hiyo imeandika dokezo kwa wahusika wenye sukari wapeleke kiasi gani kwa kila mkoa na kuwaomba watendaji wa Serikali na viongozi wenye dhamana wawasiliane na Katibu Mkuu ili awasiliane na wasambazaji waweze kupeleka sukari mikoani maana ni kweli kuna tatizo la sukari .
Alisema namna ya kutatua tatizo hilo ni viongozi wa mikoa kufuatilia na kutoa maelekezo wanahitaji tani ngapi katika mikoa yao kama walivyofanya wakuu wa mikoa ya Mwanza na Manyara.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment