Tuesday, 21 June 2016

WATUMISHI HEWA WAZIWEKA REHANI AJIRA ZA MAAFISA UTUMISHI


Serikali imeagiza wote waliotengeneza watumishi hewa wafunguliwe mashitaka mahakamani huku ikionya kuwa iko tayari kusimamisha kazi maofisa utumishi wote nchi nzima wanaofikia 1,500 katika sakata hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki alisema hayo alipokuwa akichangia mjadala wa Hotuba ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/2017 bungeni mjini Dodoma.

Amesema tayari serikali imeshatoa agizo hilo la kuwashitaki maofisa wote waliotengeneza watumishi hewa na ikibidi iko tayari kuwasimamisha kazi maofisa utumishi 1,500 waliofundishwa kazi hiyo na serikali.

Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, mpaka mwishoni mwa Mei, serikali ilikuwa imebaini uwepo wa watumishi hewa 12, 246 waliokuwa wakitafuna Sh bilioni 25.06 kila mwezi.


Katika kuelezea athari za ufujaji huo wa fedha za serikali, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema hata katika ulipaji wa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii, Rais John Magufuli aliagiza uhakiki ufanyike, kabla ya kulipa kwa kuwa penye wafanyakazi hewa, kuna malipo hewa ya wastaafu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment