Sunday, 12 June 2016

WASTAAFU 67 NA WAFU 15 WAONGEZA IDADI YA WATUMISHI HEWA IRINGA


WASTAAFU 67 na wafu 15 ni sehemu ya watumishi hewa 169 waliobainika katika taarifa mpya ya watumishi hewa mkoani Iringa iliyotolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza.

Akizungumza na wanahabari juzi, Masenza alisema idadi hiyo imebainika baada ya kuunda timu ya wataalamu waliopitia taarifa za watumishi katika hospitali teule zote za wilaya na kwenye mamlaka za serikali za mitaa.

“Timu imekamilisha kazi yake Juni 7 na kunikabidhi taarifa yake,” alisema huku akitaja kiasi cha fedha ambazo serikali imepoteza kwa kuwalipa watumishi hao kuwa ni zaidi ya Sh Milioni 360.

Wakati wastaafu wamechuma isivyo halali zaidi ya Sh Milioni 83, zaidi ya Sh Milioni 53 zililipwa kwa watumishi waliofariki na zaidi ya Sh Milioni 226.6 zililipwa kwa watumishi 87 watoro na waliofukuzwa kazi.

Akitoa mchanganuo wa watumishi hao kwa kila halmashauri, Masenza alisema watumishi hewa 90 wamebainika kuwepo katika halmashauri ya wilaya ya Mufindi, Iringa (42), Iringa Manispaa (20), Mafinga Mjini (9) na Kilolo (8).

Katika taarifa yake hiyo, Mkuu wa Mkoa alisema timu hiyo imebaini pia tatizo la fedha za mishahara isiyolipwa ya zaidi ya Sh Milioni 151.5 katika hospitali teule ya Ilula inayotoa huduma katika halmashauri ya wilaya ya Kilolo.

“Mishahara hiyo pamoja na kutolipwa haikurejeshwa hazina. Ni mishahara ya tangu Januari 2008 hadi Februari 2016,”alisema.

Alisema badala ya kulipa watumishi mishahara fedha hizo zimetumiwa na uongozi wa hospitali hiyo kwa shughuli za uendeshaji wa hospitali bila idhini ya serikali.


“Fedha hizo zilitumika kugharamia huduma za umeme, ununuzi wa dawa na kulipa mishahara ya watumishi ambao orodha yake haikuwa inafahamika na serikali kinyume na taratibu,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment