Wednesday, 22 June 2016

WANAHABARI WADHIBITIWA WAKATI MTUHUMIWA WA MAUAJI YA MWANGOSI AKIKUTWA NA KESI YA KUJIBU
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Iringa imesema mtuhumiwa wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, Daudi Mwangosi, ana kesi ya kujibu.

Mtuhumiwa huyo Pacificius Cleophace Simoni alifikishwa mahakamani hapo akituhumiwa kumuua Mwangosi kwa kukusudia katika tukio lilitokea katika kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi Mkoani Iringa Septemba 2, 2012.

Akitoa uamuzi huo jana,  Jaji wa mahakama hiyo, Paul Kiwelo alisema; “Mahakama imejiridhisha kwamba katika shauri lililoko mbele yetu, tuhuma ambazo zimetolewa dhidi ya mtuhumiwa na kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na upande wa Jamuhuri, mtuhumiwa ana kesi ya kujibu kwahiyo natupilia mbali ombi la upande wa utetezi lililotaka kesi hii itupiliwe mbali kwa madai kwamba hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja unaomuhusisha mtuhumiwa na mauaji hayo.”

Jaji Kiwelo alisema mtuhumiwa huyo ataanza kujitetea kesho baada ya kuridhia ombi hilo lililotolewa na wakili wa upande wa utetezi Lwezaula Kaijage na kuungwa mkono na mawakili wa Jamuhuri, Sandy Hyra na Ladslaus Komanya.

Mara baada ya Jaji huyo kutoa uamuzi huo, askari Polisi zaidi ya 20 waliokuwa ndani ya chumba cha mahakama hiyo, walimfunika shuka mtuhumiwa huyo ili wanahabari wasipate fursa ya kumpiga picha.

Mtuhumiwa huyo alitolewa mahakamani hapo na kundi la askari hao, akiwa amefichwa katikati yao, hatua ambayo pia iliwazuia wanahabari kufanya kazi yao vizuri.

Tofauti na watuhumiwa wengine, mtuhumiwa huyo aliyekuwa askari wa FFU Iringa kabla ya kufikishwa mahakamani hapo aliondolewa katika eneo la mahakama kwa kutumia gari dogo la Polisi aina ya Landlover badala ya kupandishwa katika kalandinga kama inavyofanywa kwa watuhumiwa wengine.

Kabla na baada ya kesi hiyo kusikilizwa baadhi ya wanahabari walilalamika kwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Ruth Massam namna baadhi ya askari waliokuwa wamevaa kiraia na sare za jeshi hilo walivyokuwa wakiwatisha wakati wakiwazuia kupiga picha.

Wanahabari hao walilalamika kwamba kila kesi hiyo inapofikishwa mahakamani hapo, kumekuwa na kawaida ya kuwepo kwa idadi kubwa ya askari wanaovaa kiraia na wale wanaovaa sare, huku baadhi yao wakiwa na silaha za moto jambo ambalo pia linawaogopesha na kuwakwamisha kufanya kazi zao kwa staha.

Akizungumzia malalamiko hayo, Msajili huyo alisema mahakama inaendelea kuyafanyia kazi huku akisisitiza shughuli za kimahakama ni shughuli zao ambazo hazipaswi kuingiliwa na mtu mwingine na kwamba atazungumza na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa ili asaidie kutoa maelekezo kwa baadhi ya askari wake wanaotaka kuingilia uhuru wa mahakama

Reactions:

0 comments:

Post a Comment