Saturday, 11 June 2016

Utambulisho NIDA kutumika kuondoa watumishi hewa

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hati wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Bi. Rose Mdami, akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Saalam. Katika kikao hicho NIDA iliwasilisha mpango usajili kufikia 31 Desemba 2016 ambapo usajili utakamilika nchini nzima na wananchi kuanza kutumia namba ya utambulisho kupata huduma. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti Mifumo ya Komputa (TEHAMA) Ndugu Mohamed Khamis, kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji Vitambulisho Ndugu Alphonce Malibiche
MAMLAKA ya Utambulisho wa Taifa (NIDA) imepanga kutumia namba ya utambulisho ili kuondoa tatizo la watumishi hewa katika taasisi na mashirika ya umma nchini. Tayari mamlaka hiyo imeshakaa na Idara ya Utumishi Serikali ili kuangalia njia rahisi ya kuwaondoa watumishi hewa kwa kutumia namba za utambulisho zitakazotolewa na mamlaka hiyo.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mifumo ya Kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Mohammed Khamis alipozungumza Dar es Salaam jana juu ya tovuti salama iliyoanzishwa na mamlaka hiyo ya kuhakikisha utambulisho.
Khamis alisema mamlaka hiyo itaunganisha kanzidata (database) yake pamoja na ile inayohifadhi taarifa za watumishi wa serikali ili kubaini watumishi hewa na taarifa zao kufikishwa katika vyombo vinavyohusika kwa hatua.
“Kila mtumishi ambaye hakupata kitambulisho cha taifa aende kwenye ofisi ya NIDA kusudi wote wawe na namba ya utambulisho. Tunatarajia hadi Agosti watumishi wote wawe na utambulisho,” alisema Khamis.
Awali, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hati, Rose Mdami alisema, tayari mamlaka hiyo imeshaanza kuzalisha vitambulisho vyenye saini ya mmiliki na mtoaji wa kitambulisho hicho.
Hata hivyo alisema vitambulisho vilivyotolewa awali ambavyo havikuwa na saini vitaendelea kutumika kama kawaida kwa kuwa muhimu ni namba ya utambulisho ambayo mtu anaweza kupata huduma mbalimbali kupitia namba hiyo.
“Mamlaka imeanza kuzalisha vitambulisho vyenye sahihi ya mmiliki na mtoaji wa kitambulisho mbele na nyuma ya sura ya kitambulisho pamoja na tarehe ya kuzaliwa. Vya zamani vitaendelea kutumika wakati tunaanda utaratibu wake,” alisema Mdami.
Mdami alisema lengo la mamlaka hiyo ni kuhakikisha hadi kufikia Desemba 31, mwaka huu watu wote wanapata utambulisho. Alisema kwa sasa watakuwa wakitumia taarifa za wananchi ambazo ziko katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kuzichakata na kutoa utambulisho.
Alisema kwenye taarifa za NIDA kuna vipengele 74 wakati NEC kuna vipengele 32 hivyo watatumia taarifa za NEC ili kutoa utambulisho, lakini ili mtu aweze kupata utambulisho kamili ni lazima ajaze vipengele vilivyobaki. “Kwa kutumia mifumo ya NEC ni kuondoa usumbufu kwa wananchi wa kukusanya taarifa upya.
Lakini mashine zetu zina uwezo wa kuzalisha vitambulisho 24,000 hivyo ukipiga hesabu kwa idadi ya Watanzania wote ambao hawana utambulisho hatuwezi kukamilisha hadi kufikia Desemba 31, mwaka huu,” alisema Mdami.
Alisema wamepokea mashine 5,000 kutoka NEC na wao walikuwa na mashine 1,500 hivyo kwa sasa wana mashine 6,500 ambazo zimeshaanza kusambazwa katika wilaya zote nchini ili kuanza kufanya kazi.
Mdami alifafanua kuwa utambulisho ni muhimu na ndio sababu kwa sasa wanafanya mchakato hadi kufikia mwisho wa mwaka kila mmoja aweze kuwa na utambulisho ambao ataweza kuutumia katika mambo mbalimbali.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment