Sunday, 12 June 2016

TANROADS IRINGA WAANZA KUZIHIFADHI HIFADHI ZA BARABARA IRINGA
Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoa wa Iringa imeanza kupanda miti katika maeneo ya hifadhi ya barabara za lami mkoani hapa katika shughuli iliyozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza juzi.

Wakianzia Kihesa Kilolo, mjini Iringa watumishi wa Tanroads na wadau wao wa barabara walipanda miti kwenye eneo lenye urefu wa kilomita 2.8 katika hifadhi ya barabara ya Iringa Dodoma.

Meneja wa Tanroads mkoa wa Iringa, Mhandisi Daniel Kindole alisema zoezi la upandaji miti litakuwa endelevu likilenga kutunza mazingira katika hifadhi ya barabara katika maeneo yote yenye barabara za lami zilizokamilika.

“Tumeanza na eneo hili la Kihesa Kilolo katika kipindi hiki cha kiangazi kwasababu liko jirani na vyanzo vya maji,” alisema na kuongeza kwamba kazi kubwa ya upandaji miti katika barabara hizo utaendelea kwa nguvu kubwa wakati wa masika.

Alisema hifadhi ya barabara ni eneo lililopembezoni mwa barabara kila upande ambalo limetengwa na kuwekwa kisheria lengo kuu likiwa ni kwa ajili ya upanuzi, ujenzi au kwa matumizi wakati wa matengenezo ya barabara.

Akizindua zoezi hilo, Mkuu wa Mkoa alisema suala la kutunza mazingira ni suala la kila mtu lenye manufaa makubwa kwa watanzania.

“Niwapongeze Tanroads kwa kuja na wazo hili litakaroboesha mazingira na kusaidia kulinda hifadhi ya barabara isivamiwe kwa shughuli zingine,” alisema.

Pamoja na kupanda miti alisema mazingira ya barabara yanapaswa kutunzwa kwa kuzingatia sheria ya barabara Na 13 ya mwaka 2007 pamoja na kanuni zake za mwaka 2009 zinazozuia kufanya kazi za gereji, kutupa taka ovyo, kuwasha moto, kukata miti, kulima na kuchimba mchanga au kokoto.


Mwenyekiti wa Kikundi cha Kutunza Mazingira Kihesa Kilolo (KIUMAKI) kilichopewa kazi ya kuimwagilia miti hiyo mpaka kipindi cha masika, Mbonea Ngwinzila alisema kwa kupitia makubaliano yao na Tanroads watahakikisha miti iliyopandwa katika eneo hilo inatunzwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment