Friday, 10 June 2016

Serikali yaanza kuyabana mashirika yake


MASHIRIKA yote na taasisi za umma pamoja na kampuni zenye ubia na Serikali, zimetakiwa kuhakikisha kila mwaka zinatoa gawio katika kuongeza mapato katika Bajeti. Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, wakati akipokea gawio la Sh bilioni 23 kutoka kampuni tatu zenye ubia na Serikali.
“Nimeagiza (mashirika, taasisi za umma na kampuni zenye ubia na serikali) yahakikishe yanatoa gawio angalau kuanzia mwakani, kwa kuwa haina maana wanatumia mtaji wetu, fedha za wananchi masikini, halafu hawatoi gawio,” alisema.
Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru ambaye ofisi yake ina jukumu la kusimamia mtaji wa serikali katika mashirika hayo, alisema mwaka huu mashirika na taasisi za umma na kampuni zenye ubia na serikali, katika Bajeti ya Serikali mwaka huu, yamepangiwa kupeleka Sh trilioni 1.3.
Pia amezitaka taasisi hizo kufikisha lengo la makusanyo na serikali itafuatilia utendaji wao ambapo yatakayoshindwa kutoa gawio, hatua zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuondoa menejimenti na bodi, ili waingie watu watakaoendesha kwa faida na kuipatia serikali gawio.
Kampuni ya kwanza kutoa gawio ilikuwa Puma Energy Tanzania Limited ambayo serikali ina hisa asilimia 50 na baada ya kupata faida ya Sh bilioni tisa, Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni hiyo, ikapendekeza gawio la Sh bilioni 4.5 kwa Serikali, ambayo ilikabidhiwa jana.
Akizungumza kabla ya kukabidhi gawio, Mwenyekiti wa Bodi ya Puma, Dk Ben Moshi alisema mwaka jana walitoa Sh bilioni tatu na mwaka huu kutokana na mazingira mazuri ya kibiashara, faida iliongezeka na kuwawezesha gawio hilo.
Alifafanua kuwa kampuni hiyo ya Puma ni ya ubia na serikali, lakini serikali ndiyo inayoonekana zaidi kwa kuwa na mali nyingi za kampuni hiyo. Alimkumbusha Waziri Mpango kuhusu agizo alilotoa juzi katika hotuba ya Bajeti la kutaka serikali itoe kipaumbele katika kufanya kazi na mashirika, taasisi za umma na kampuni zenye ubia na serikali.
Mwenyekiti huyo wa Puma alisema serikali imemuwahi katika hotuba hiyo, kwa kuwa walipanga kuomba mashirika ya umma yafanye biashara na serikali. Alitoa mfano wa kituo kimoja kinachotumika kuuzia mafuta magari ya serikali kwamba kama kazi hiyo ingepewa Puma, huenda gawio lingekuwa kubwa zaidi.
Kwa mujibu wa Dk Moshi, mbali na kampuni hiyo kuwa na ubia na serikali, lakini ndiyo kampuni inayouza mafuta yaliyo bora na imeshinda tuzo moja ya dunia ya ubora wa mafuta ambapo ilikuwa ya kwanza na kufuatiwa na kampuni kutoka Vietnam. Pia ilishinda tuzo ya utunzaji wa mazingira.
Changamoto ya pili aliyoieleza Dk Moshi, ni upotevu wa mafuta wakati wa kuyatoa katika meli kuingiza kwenye bomba la kwenda katika matangi ya Puma, ambapo walijikuta wakipoteza mafuta yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1.4, sawa na karibu Sh bilioni 3.
Tipper inayofanya biashara ya kutoa hifadhi ya mafuta ambayo Serikali inamiliki asilimia 50 ya hisa, nayo ilikabidhi gawio la Sh bilioni mbili. Mwenyekiti wa Bodi ya Tipper, Profesa Abdulkarim Mruma, alisema mwanzoni walikuwa na uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo 110,000 lakini waliongeza uwezo na sasa wanao uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo 213,000.
Alisema kampuni hiyo ina uwezo wa kupakua mafuta yanayofikia tani 90,000 kwa siku mbili tu tofauti na kampuni ndogondogo, ambazo upakuaji wao huchukua siku nane na kusababisha kuingia gharama za tozo ya ucheleweshaji meli.
Profesa Mruma alisema pia mafuta yanayopakuliwa Tipper, huingia katika tangi moja na kuondoa hatari iliyopo ya kubadilisha mabomba kutoka tangi moja kwenda lingine na kutoa urahisi kwa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA), kukadiria mapato.
Benki ya NMB ambayo serikali inamiliki hisa ya asilimia 31.9 nayo imekabidhi gawio la Sh bilioni 16.5, ambapo Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Ineke Bussemaker, alisema pamoja na mafanikio ya mwaka uliopita yaliyowawezesha kupata faida, kuna fursa bado ya mafanikio zaidi.
Alisema serikali ni mmoja wa wateja wakubwa wa benki hiyo na wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na katika mpango wao, wanatarajia kuongeza wateja kutoka milioni mbili mpaka kufikia milioni nne katika miaka mitano.
Akizungumza baada ya kupokea gawio la kila kampuni, Dk Mpango alimuagiza Mafuru kufuatilia mashirika na taasisi zote za umma na kampuni ambazo serikali zina hisa kuhakikisha zinatoa gawio kwa serikali angalau mwaka huu.
Alihakikishia kampuni za Puma na Tipper kuwa changamoto walizotoa, zitafanyiwa kazi na baadhi zilishaanza kufanyiwa kazi, kwa kuwa Serikali inataka kupata gawio kubwa zaidi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment