Thursday, 30 June 2016

Serengeti Boys waenda Shelisheli leo


KIKOSI cha timu ya soka ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys kinatarajiwa kuondoka leo kwenda Shelisheli kwa ajili ya mchezo wa marudiano utakaochezwa keshokutwa Julai 2.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) Alfred Lucas alisema kuwa timu hiyo itaondoka na kikosi cha wachezaji 20 pamoja na benchi la ufundi la watu watano na mkuu wa msafara ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ayoub Nyenzi.
“Timu inatarajiwa kuondoka kesho (leo) alfajiri na msafara wa watu 27 kwa ajili ya mchezo wa kutafuta kufuzu fainali za Afrika, hivyo watanzania mnaombwa kuombea timu yetu ifanye vizuri, kwani ndio timu pekee iliyobaki kwenye mashindano”, alisema Lucas.
Serengeti Boys inakwenda kucheza na Shelisheli ikiwa inahitaji ushindi wa aina yoyote au sare ili kusonga hatua ya pili kwani mchezo wa awali iliifunga Shelisheli mabao 3-0.
Endapo Serengeti Boys itafanikiwa kuiondoa Shelisheli itakutana na timu ya vijana ya Afrika Kusini.
Naye kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Shime, alisema kikosi chake kipo kamili kwa ajili ya mchezo huo kwani dosari zilizojitokeza kwenye mchezo wa awali wamezifanyia kazi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment