Monday, 27 June 2016

Serengeti Boys -3 Shelisheli -0

TIMU ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’, jana ilianza kwa kishindo harakati za kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana wa umri huo mwaka 2017, baada ya kushinda mabao 3-0 dhidi ya Shelisheli.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Serengeti ilitawala vipindi vyote vya mchezo huo na kuwazidi mbinu wapinzani wao waliokuwa wakicheza mchezo wa kuzuia muda wote.
Serengeti ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 15 kupitia kwa Nickson Clement baada ya kuunganisha mpira wa kona uliopigwa na Asad Juma.
Ibrahim Ally aliifungia Serengeti bao la pili katika dakika ya 22 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa wa Shelisheli, Juninho Mathiot na kuujaza mpira wa wavuni.
Katika kipindi hicho cha kwanza Serengeti Boys ilitawala mchezo huo na washambuliaji wake waliliandama lango la Shelisheli iliyocheza mchezo wa kuzuia karibu muda wote wa kipindi hicho.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Serengeti ilipata bao la tatu katika dakika ya 62 lililofungwa na Ally Msengi kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi Belay Asserese wa Ethiopia baada ya mchezaji Jesus Joseph wa Shelisheli kushika mpira eneo la hatari.
Aidha katika kipindi hicho cha pili Shelisheli walionekana kuzinduka dakika za mwisho na kutengeneza nafasi nyingi lakini washambuliaji wake walishindwa kufunga.
Serengeti Boys: Ramadhan Kabwili, Israel Mwenda, Nickson Kibabage, Nickson Job, Ally Msengi, Ally Hamisi, Kelvin Naftal, Shaaban Ada, Ibrahim Ali, Rashid Chambo, Asad Juma.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment