Tuesday, 21 June 2016

POLISI WAENDELEA KUMSAKA ASKOFU GWAJIMAPolisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema inaendelea kumtafuta Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kwa ajili ya kumhoji kuhusu mahubiri yenye dalili za kichochezi aliyoyatoa wiki moja iliyopita.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro amewaambia wandishi wa habari kuwa jeshi hilo bado linaendelea kumtafuta na endapo mtu yeyote ana taarifa za alipo askofu huyo, asisite kupeleka taarifa Polisi ili akamatwe.

Askofu Gwajima anatafutwa na jeshi hilo kwa ajili ya kuhojiwa juu ya mahubiri yake aliyoyatoa Juni 11, mwaka huu kanisani kwake Ubungo Maji jijini Dar es Salaam. Katika mahubiri hayo ambayo yalisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, askofu huyo alisikika akiukosoa utendaji kazi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Pia Gwajima alisikika akimshauri Rais John Magufuli, kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) iwapo watakataa kumkabidhi uenyekiti na kwamba apeleke muswada bungeni, kuondoa kinga ili rais ashtakiwe kwa makosa aliyoyafanya akiwa madarakani.


Tangu juzi Jumapili, Juni 19, Askofu Gwajima hakuonekana nyumbani kwake wala kanisani kwake na jeshi la polisi limekua likifanya doria maeneo hayo ili wamkamate lakini imeshindikana.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment