Wednesday, 15 June 2016

Pluijm aionya CAF

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm (katikati) akiwapa maelekezo wachezaji wake wakati wa mazoezi yao juzi nchini Uturuki. (Na Mpigapicha Maalumu).
KOCHA Mkuu wa Yanga Hans Pluijm ameliomba Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kuchukua hatua kali kwa klabu ambayo mashabiki wake wataleta vurugu kwa timu pinzani kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC).
Yanga itakuwa mgeni wa klabu ya Mo Bejaia kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya mashindano ya CAFCC mwishoni mwa wiki hii nchini Algeria. Pluijm mwenye uzoefu wa mashindano makubwa Afrika, alisema katika mahojiano maalumu na gazeti hili kwa njia ya mtandao kuwa kwa miaka mingi kumekuwa na vitendo vya vurugu kwenye soka la Afrika, ambapo timu mwenyeji imekuwa ikiifanyia timu ngeni.
Alitolea mfano wa vurugu ambazo Yanga walifanyiwa kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri ugenini na dhidi ya Sagrada Espranca nchini Angola na kusema vitendo hivyo havina budi kukomeshwa.
“Vitendo vya vurugu dhidi ya timu ngeni katika soka la Afrika sio vya sasa, vipo kwa miaka mingi sana. Sisemi natarajia kukutana navyo katika mchezo dhidi ya Mo Bejaia au la, lakini tunatakiwa kujiandaa kisaikolojia kwa lolote.
“CAF wanapaswa kuwa wakali dhidi ya vitendo hivi vya vurugu vinavyofanywa na timu wenyeji kwa wageni wao. Wanatakiwa kuchukua hatua kali,” alisema Pluijm ambaye yuko na timu yake nchini Uturuki ikijiandaa na mchezo huo.
Pluijm alisema kwenye hatua hiyo wanaziheshimu timu zote walizopangwa nazo, lakini hawazihofii na huo ndio mpango wao kukabiliana na wapinzani wao. Naye Vicky Kimaro anaripoti kuwa, timu ya Yanga imeendelea na kambi yake ya mazoezi nchini Uturuki, ambapo Pluijm amewaanzishia programu maalumu ya mazoezi usiku na hiyo ni kutokana na taarifa kuwa mchezo wao utafanyika usiku.
Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuwakaribisha mabingwa wa Afrika, TP Mazembe Juni 28 katika mchezo wake wa pili wa Kundi A. Timu nyingine Kundi A ni Medeama ya Ghana ambayo itafungua dimba na TP Mazembe mjini Lubumbashi Juni 17, mwaka huu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment