Saturday, 25 June 2016

Nyota wa zamani waionya Yanga CAF


Kikosi cha Yanga.
WACHEZAJI wa zamani wa Yanga na Simba wameitaka Yanga kutobweteka katika mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe na badala yake watulie na kutumia vyema uwanja wa nyumbani kupata matokeo mazuri.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, wachezaji hao walisema Yanga ilionesha kandanda nzuri katika mchezo dhidi ya Mo Bejaia isipokuwa safu ya ushambuliaji haikucheza kwa utulivu.
Miongoni mwa wachezaji hao ni Mwanamtwa Kihwelu na Moses Mkandawile waliosema kuwa Yanga inaweza kupata matokeo mazuri iwapo kama hawatabweteka, na ikiwa watapambana kwa ushirikiano.
Kihwelu alisema: “TP Mazembe sio timu nyepesi kwani ina uzoefu wa mashindano hayo, na tayari wana pointi tatu na kuhimiza Yanga kutulia kwenye uwanja wa nyumbani kutengeneza nafasi zenye kuzaa matunda.”
Alisema kinachohitajika ni mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuzidisha mara mbili kiwango chao ili kuwa na uhakika wa kuibuka na ushindi. Kihwelu alipendekeza kuwa iwapo Juma Abdul na mchezaji mpya Obrey Chirwa watakuwepo kuna uwezekano wa kupata ushindi mzuri.
Kwa upande wake, Mkandawile aliwahimiza Yanga kucheza wakijua kuwa wako kwenye uwanja wa nyumbani. Alisema ni muhimu kuzingatia nidhamu kwa ajili ya kuepukana na kadi nyingi zisizokuwa na tija .
Golikipa huyo wa zamani wa Simba alisema sehemu inayohitaji kufanyiwa kazi ni safu ya ulinzi na ushambuliaji, kwani wanahitaji kucheza kwa utulivu mkubwa. Yanga wanatarajiwa kushuka dimbani Juni 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa pili hatua ya makundi. Kwa sasa wanaendelea kujifua na mazoezi katika kambi yao iliyoko nje ya nchi Uturuki na kesho wanatarajiwa kurudi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment