Thursday, 30 June 2016

Nangole wa Chadema avuliwa ubunge Longido

 
Aliyekwa Mbunge wa Jimbo la Longido,Mh.Onesmo Nangole
MBUNGE wa Longido, Onesmo ole Nangole (Chadema) amekuwa mbunge wa kwanza kupoteza jimbo lake baada ya jana Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kutengua matokeo ya Uchaguzi Mkuu na kuamuru urudiwe.
Jaji Mfawidhi Kanda ya Bukoba, Sivangilwa Mwangesi ametengua matokeo hayo baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 27 huku aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi, Felix Kimario ushahidi wake kuonesha kulikuwa na udanganyifu katika katika matumizi ya fomu ya matokeo ya udiwani na ubunge.
Uamuzi wa kutengua matokeo ya ubunge wa jimbo hilo la Longido ni wa kwanza miongoni wa kesi za uchaguzi zinazonguruma katika mahakama mbalimbali nchini.
Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, Nangole aliyejiunga na Chadema baada ya kuihama CCM alikokuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, alimshinda mgombea wa CCM, Dk Stephen Kiruswa kwa kura 20,076. Kiruswa alipata kura 19,352, hivyo kufanya tofauti ya kura 724 tu.
Katika hukumu yake, Jaji Mwangesi alisema kulikuwa na maigizo mbalimbali katika kujaza fomu za matokeo ya uchaguzi kwani fomu iliyotumika kujaza matokeo ya uchaguzi wa mbunge ilitumika ya udiwani.
Alisema fomu namba 21 (c) iliyotakiwa kujazwa matokeo ya udiwani ilifutwa kiaina na kujazwa kuwa ni namba 21 (b) ambayo ndio iliyotumika kujaza matokeo ya ubunge.
Pia Jaji Mwangesi alisema katika chumba cha utangazaji wa matokeo ya ubunge kulikuwa na fujo zilizotokea na kusababisha kuvurugika kwa ujumlishaji wa matokeo, na purukushani zilizosababisha Nangole kumwagia maji baadhi ya fomu muhimu za matokeo katika kata mbalimbali ikiwa ni njama za kutaka kuharibu matokeo.
Aidha, alisema Kimario alishindwa kuithibitishia mahakama katika ushahidi wake kwa nini fomu ya matokeo ya udiwani itumike kujaza matokeo ya ubunge, na kwamba aliomba mahakama kuona kuwa hakukuwa na njama zozote za kubadilisha matokeo bali na kasoro kama kasoro wanavyofanya binadamu.
Alisema mahakama imejiridhisha katika kipindi cha kampeni kulikuwa na lugha chafu, kashfa, ubaguzi na matusi na upande wa mshitakiwa umeshindwa kujitetea kama kweli madai hayo hayakuwa ya kweli.
Jaji Mwangesi alisema mahakama imebaini kuchanganywa fomu za madiwani na ubunge kulikuwa na lengo la kuharibu matokeo ya uchaguzi na ndiko kulikomwezesha Nangole kushinda ubunge, hivyo ni ubatili wa makusudi.
Katika kesi hiyo iliyosikilizwa kwa zaidi ya miezi mawili, Jaji Mwangesi ametengua matokeo ya uchaguzi huo, akisema yalikuwa batili na kumuamuru Mkurugenzi wa Uchaguzi kutangaza tarehe ya marudio ya uchaguzi na mlalamikiwa namba moja (Ole Nangole) anapaswa kulipa gharama za kesi.
Baada ya Jaji Mwangesi kutoa hukumu hiyo, shangwe na nderemo zikiambatana na vifijo, vilitawala ndani ya chumba cha mahakama wakati jaji akijiandaa kutoka huku furaha za wanachama wa CCM wakifurahi na kumkumbatia aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Kiruswa kwa ushindi huo.
Akizungumzia uamuzi huo, Dk Kiruswa aliipongeza mahakama kwa kuona kasoro, hila na hujuma mbalimbali katika uchaguzi Jimbo la Longido huku akimshukuru Mungu na mashahidi na wakazi wa Longido waliokuwa nyuma yake katika kesi hiyo.
Naye Nangole alisema atachukua hatua kwa uamuzi huo, lakini hakutaja hatua hiyo, huku akiwa amezungukwa na wafuasi na viongozi wa Chadema kutoka Longido, Monduli na Arusha Mjini walioonekana kunywea kwa uamuzi huo.
Aidha, nje ya mahakama baadhi ya wafuasi wa Chadema hawakuamini matokeo hayo, huku wengine walipata mshituko na kuzirai, ilhali wenzao wakiendelea na shangwe za kila aina.
Kiruswa alimshitaki Nangole, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Longido akilalamikia kuvurugwa kwa matokeo, fujo katika kuhesabu na kashfa na matusi katika kampeni.
Alitetewa na Dk Masumbuko Lamwai akisaidiwa na Edmund Ngemela na Daudi Haraka, huku Nangole akitetewa na Wakili Method Kimomogolo akisaidiana na John Materu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali akiwakilishwa na Daudi Akway akisaidiana na Neema Mwanga na Fortunatus Mhalila.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment