Thursday, 16 June 2016

MWENYEKITI WA CCM MKOA WA IRINGA ATOA MSAADA WA MADAWATI


MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Dk Jesca Msambatavangu ametoa msaada wa madawati 50 yenye thamani ya Sh Milioni 2.5 kwa ajili ya shule ya Msingi ya Igwachanya iliyopo kata ya Mseke, nje kidogo ya manispaa ya Iringa.

Dk Msambatavangu alikabidhi madawati hayo juzi akisema anaunga mkono wito wa serikali ya Dk John Magufuli inayotaka tatizo la madawati katika shule zote za msingi liwe limamalizika ifikapo, Juni 30, mwaka huu.

“Nitoe wito kwa wanasiasa wenzangu, wafanyabiashara, wakulima, wafanyakazi na wadau wengine wote wa maendeleo mkoani Iringa, mahali popote walipo waone tatizo la watoto wetu kukaa chini ni tatizo letu sote linalopaswa kushughulikiwa kwa nguvu zetu wote,” alisema.

Alisema mpango wa serikali wa kutoa bure elimu ya msingi hadi sekondari hauna maana wadau wa sekta hiyo wasishiriki kuchangia maendeleo ya shule hizo.

“Msingi wa sera ya elimu bure unazuia kuwalazimisha wanafunzi, wazazi na walezi wao kuchangia shughuli mbalimbali zinazohiji fedha katika shule zao lakini hauzuii wadau kwa kujitolea kushiriki kuchangia maendeleo ya shule hizo,” alisema.

Akipokea msaada huo, Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Charles Matunduru alisema utasaidia kupunguza tatizo la idadi ya madawati yanayopungua katika shule mbili za msingi za kijiji hicho.

“Kabla ya msaada huu, upungufu wa madawati katika shule ya Ugwachanya ulikuwa 170 na shule ya msingi Kipanga ni 46. Tumepokea msaada kutoka kwa Dk Jesca na wadau wengine na kufanya upungufu hadi sasa kwa shule zote mbili uwe madawati 106,” alisema.

Pamoja na shule hizo kukabiliwa na upungufu wa madawati hayo, alisema miundombinu yake yakiwemo majengo ni mibovu ikiwa haijakarabatiwa kwa muda mrefu.


Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho Juma Mwakawago alimshukuru mwenyekiti huyo akisema ni kiongozi wa mfano wa kuigwa katika jamii ambaye siku zote anapoombwa kuchangia maendeleo ya watu wengine amekuwa akifanya hivyo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment