Friday, 3 June 2016

Makinda aahidi `Kazi Tu’ NHIF

MWENYEKITI mpya wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Anne Makinda
 MWENYEKITI mpya wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Anne Makinda ametembelea makao makuu wa Mfuko huo na kusema pindi bodi itakapoanza kufanya kazi, watatekeleza majukumu yao katika kuhakikisha mfuko unafikia malengo ya kuhudumia wananchi.
Wiki moja iliyopita, Rais John Magufuli alimteua aliyekuwa Spika wa Bunge, Makinda kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF baada ya ile ya awali iliyokuwa ikiongozwa na Balozi Ali Mchumo kumaliza muda wake tangu mwaka jana.
Akizungumza na uongozi wa NHIF na kujionea utendaji kazi, Makinda alisema; “Leo nimekuja kujifunza, nimefanya kazi ya kusikiliza tu. Nashukuru Waziri (Ummy Mwalimu) ameteua wajumbe, Bodi ikizinduliwa tutaanza kazi tunayotakiwa kufanya ya kuhakikisha Mfuko unatekeleza majukumu yake ipasavyo.”
Akizungumza jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema mfuko umefarijika kupata bodi mpya chini ya Makinda ambaye ni mchapakazi na ana imani uongozi huo utasaidia kuondoa changamoto za mfuko na kuhakikisha unatekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Alisema kwa sasa mfuko una changamoto kubwa ya mwitikio mdogo wa kujiunga na kuwa kwa sasa wamefikia asilimia 29 na kuwa lengo ni kufikisha zaidi ya asilimia 50 miaka michache ijayo, sambamba na kuridhisha wanachama wao kwa kutoa huduma iliyo bora.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment